VIONGOZI wa Vyama vya Ushirika nchini wametakiwa kutumia njia mbadala kulipa madeni ya wanaushirika badala ya kuuza mali ili kulipa madeni hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alieanza ziara ya kikazi ya siku tatu leo ( 18.02.2021) mkoani Kilimanjaro ambapo amebaini changamoto ya uwepo wa madeni katika vyama vingi vya ushirika hapa nchini yaliyosababishwa na matatizo ikiwemo kukosekana kwa weledi miongoni mwa viongozi wa ushirika.
Akiongea na bodi pamoja na menejimenti ya kiwanda cha kahawa cha Moshi (TCCco )Kusaya amesema vyama vingi vya ushirika vinadaiwa na watumishi wake kwa kutolipa mishahara kwa muda mrefu hivyo ushirika utafute njia mbadala ya kulipa madeni hayo badala ya kufikiria kuuza majengo ya ushirika na Mali zingine.
"Tutafute namna bora ya kulipa madeni ya wanaotudai kwa kuwa suluhu sio kuuza majengo siamini kwamba kila anayedai tunauza jengo wakati kila mwaka atastaafu mtumishi tutauza majengo mangapi alihoji" Katibu Mkuu Kusaya.
Hata hivyo ,Kusaya ametoa wito kwa kila Chama cha ushirika kilinde mali zake kwa ajili ya watu wake
Katika kuhakikisha vyama vya ushirika nchini vinatekeleza wajibu wake Kusaya amewataka wataalamu wa fedha kuhakikisha kwamba kila deni litakalolipwa kwa mtumishi wa ushirika linakaguliwa na kubainika kwamba ni deni sahihi.
"Wataalam wa fedha ni sharti wajiridhishe na uhalali wa madeni kwenye ushirika kabla malipo hayajafanyika ili kuepuka madeni hewa ambayo Rais Dkt. John Pombe Magufuli anapambana kuyadhibiti kwa maslahi ya wanaushirika wakiwemo wakulima" alisisitiza Kusaya.
Katibu Mkuu huyo wa Kilimo yupo kwenye ziara ya kikazi kukagua utendaji kazi wa vyama vya ushirika na kuhimiza Kilimo cha umwagiliaji na kuzungumza na watumishi wakiwemo wakulima wa mazao mbalimbali ili kutatua changamoto zinazowakabili.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments