Mawaziri wa nchi tajiri za kundi la G7 wanaanza mkutano wao jijini London nchini Uingereza. Mawaziri hao watajadili juu ya uwezekano wa kuzitoza kodi zaidi kampuni kubwa kabisa duniani.
Mawaziri hao wa fedha wa nchi saba tajiri G7 wanaanza mkutano wa siku mbili mjini London kujadili njia za kufikia mkataba wa kimataifa juu ya kuongeza kodi kwa kampuni kubwa, ikiwa ni pamoja na kampuni za mitandao za Google, Facebook na Amazon.
Mkutano huo unaofanyika chini ya uenyekiti wa waziri wa fedha wa Uingereza Rishi Sunak unawakutanisha mawaziri hao ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu kuzuka janga la corona. Waziri wa fedha wa Uingereza Sunak amesisitiza umuhimu wa kukutana ana kwa ana na mawaziri wenzake kutoka Marekani, Japan, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Canada kwenye mazungumzo hayo ya siku mbili.
Waziri wa Fedha wa Uingereza Rishi Sunak
Waziri Sunak ameelezea matumaini ya kupatikana makubaliano kwenye mkutano huo hasa kutokana na dhamira ya rais wa Marekani Joe Biden ya kutaka kampuni kubwa duniani zitozwe kodi zaidi. Hata hivyo changamoto kubwa ni namna ya kufikia makubaliano juu ya kuleta mageuzi katika mfumo wa kodi. Makubaliano hayo yatapaswa kuwasilishwa kwenye mkutano wa kundi la nchi za G20 utakaofanyika mwezi ujao nchini Italia.
Marekani imependekeza kiwango cha chini kuwa ni asilimia 15 kwa kampuni 100 kubwa kabisa duniani. Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire amesema inapasa kufikia makubaliano. Amesisitiza kwamba hiyo itakuwa hatua muhimu. Hata hivyo waziri wa fedha wa Japan Taro Aso amesema ana mashaka iwapo makubaliano yatapatikana kwenye mkutano huo wa mjini London.
Kwa upande wake Marekani inatarajia makubaliano kamili kupatikana kwenye mkutano utakaohudhuriwa na marais na mawaziri wakuu wa kundi la nchi wanachama wa G20 utakaofanyika nchini Uingereza kuanzia tarehe 11 hadi 13 mwezi huu.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf ScholzWaziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf Scholz
Nchi zote zitanufaika ikiwa kampuni kubwa zinalipa kodi zaidi pale ambako zinafanya kazi na kuingiza fedha na siyo tu pale ziliposajiliwa au kwenye makao yake makuu. Marekani inataka kuondolewa kwa kodi ya huduma za kidijitali inayotozwa nchini Uingereza, Ufaransa na Italia. Marekani imelalamika kwamba sera hiyo inayalenga makampuni yake. Ikiwa makubaliano hayatafikiwa juu ya kodi hiyo ya kimataifa, bidhaa za anasa kutoka Uingereza, Italia na Uhispania zitakuwamo hatarini kutozwa ushuru wa asilimia 25 nchini Marekani baadae mwaka huu.
Ujerumani,Uingereza na Ufaransa ziko tayari kukubaliana na pendekezo la Marekani lakini zinataka kampuni kubwa kama ya Amazon nayo iingizwe katika mfumo huo wa kodi. Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kampuni zote, bila ya walakini zitapaswa kufuata sheria mpya.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments