SERIKALI SINGIDA YAKAMATA MALORI YENYE TANI 40 ZA MAZAO YASIYO LIPIWA USHURU | ZamotoHabari.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili akikagua moja ya lori lililokamatwa na shehena ya maharage ambayo yanadaiwa kutolipiwa ushuru.

Mfanyabiashara wa maharage , Philipp Lehema akizungumza na Mkuu wa Wilaya Paskas Muragili baada ya kukamatwa kwa maharage hayo.

Mkaguzi wa mazao katika Kituo cha Njia Panda, Juma Athumani akitoa maelezo kwa  DC Muragili jinsi alivyo yakamata magari hayo.

Malori yaliyokamatwa na mzigo huo.

Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Hassan Ngoma  (katikati) akizungumzia tukio hilo.

DC Muragili  (kushoto) akizungumza na dereva Moses Zelothe ambaye gari lake lilikamatwa na mchele ambao haukulipiwa ushuru.
Diwani Mstaafu Hamisi Labu akiipongeza Serikali kwa kuyakamata magari hayo na kuwaomba wafanyabiashara kujenga tabia ya kulipa ushuru wa mazao pasipo shuruti.


Na Dotto Mwaibale, Singida



SERIKALI mkoani Singida imekamata malori matano yenye magunia ya mazao mchanganyiko zaidi ya tani 40 yaliyokuwa yakipitia mkoani hapa bila ya kuwa na nyaraka zozote za kulipia ushuru.

Kufuatia kukamatwa kwa shehena hiyo Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili aliagiza Wafanyabiashara hao  waliokuwa wakisafirisha shehena hiyo ya mazao  kutozwa faini ya sh.milioni 4.5 ukiwemo ushuru.

"Faini kwa Mfanyabiashara wa maharagwe, Philipp Lehema ni sh.milioni 4 na mwenzake Moses Zelothe ni sh.500,000." alisema Mulagiri.

Akifafanuaa kuhusu faini hizo Mulagiri alisema kwa kosa la kudanganya kuhusu ulipaji huo Lehema alitozwa faini ya sh.200,000 kwa kila gari kati ya manne  yaliyokuwa na mzigo huo na kutakiwa kulipa ushuru wa sh.3000 kwa magunia 1200.

Alisema  kwa mfanyabiashara Zelothe alitozwa faini ya sh. 200,000 kwa gari lake na sh. 300,000 kwa magunia 150 ya mchele ambayo hakuyalipia ushuru.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Muragili alisema shehena hiyo ya mazao aina ya maharage na mchele ilikuwa ikisafirishwa kutoka mkoani Kagera na Tabora kwenda Arusha.

Alisema shehena hiyo ilikamatwa ikisafirishwa kwenye malori matano,  manne yenye maharage yakiwa ya Lehema na lenye pumba na mchele likiwa la Zelothe.

Alitaja namba za malori hayo kuwa ni T 335 AWH, T 178 CBB, T 662 DTL, T 489 DUV na T 850 AFQ.

Alisema wafanyabiashara waliokamatwa wakisafirisha shehena hiyo walikuwa wakitumia stakabadhi za malipo ya maegesho ya magari wakati wakipakia mazao hayo kukwepa ushuru.

Mfanyabiashara Philipp Lehema ambaye alikuwa akisafirisha maharage hayo alikiri kusafirisha bidhaa hiyo kwa kutumia stakabadhi ya ushuru wa maegesho na ameshangaa kuona akikamatwa kwa madai ya kutolipa ushuru wakati yeye alifahamu ameshalipia ushuru huo kwa kutumia stakabadhi hizo.

Muragili alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wafanyabiashara wenye tabia  ya kukwepa kulipa ushuru kwa visingizio mbalimbali na kwamba kwa Mkoa wa Singida hawatapita watakamatwa. 

Mkaguzi wa mazao katika Kituo hicho cha Njia Panda kilochopo wilayani humo,  Juma  Athumani alisema baada ya kuyakamata magari hayo wahusika wenye mzigo huo walijaribu kumshawishi hayaruhusu magari hayo lakini aliwakatalia kwa kuwa alijua kufanya hivyo ilikuwa ni kuikosesha Serikali mapato.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa amempongeza mkaguzi huyo na wenzake waliokuwa zamu siku hiyo kwa kuwa na moyo wa kizalendo na ameahidi kuwapa motisha.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini