Na Hamida Kamchalla, TANGA
BAADHI ya Walimu na Wazazi wenye watoto viziwi jijini Tanga wameiomba Serikali kufanya utaratibu na kuangalia namna ya kuweza kutenga madarasa ya wanafunzi wenye ulemavu kutokana na ufundishaji wa Elimu Jumuishi kuwawia mgumu walimu na wanafunzi.
Rai hiyo imetoĺewa jana wakati wa majadiliano ya changamoto za wenye ulemavu mashuleni ambapo imeonelewa kwamba wanafunzi hao wanashindwa kufanya vizuri katika masomo yao kuanzia kidato cha kwanza kutokana na ugumu wa ufundishajo kwa walimu hasa lugha ya alama.
Wamefafanua kwamba wanafunzi shule za msingi kwa sasa wamegawiwa madarasa watoto wanafaulu wakifika sekondari wanakumbana na changamoto ya kuchanganywa hali inayowapa shida hata walimu kwani wengi hawajui lugha ya alama hivyo kupelekea kufeli katika masomo yao.
"Elimu jumuishi ni kikwazo kikubwa mashuleni, sisi Walimu tunapendekeza hilo suala la elimu jumuishi lifanyiwe marekebisho, sisi walimu, tunataka wanafunzi viziwi nao wafaulu kama watoto wengine, kama msingi iliwezekana kuwatenga madarasa serikali inashindwa nini kwa sekondari" alisema Mwalimu wa sekondari Old Tanga, Bob Lyatuu.
Kwa upande wake wa Mwenyekiti CHAVITA Taifa Nidrosy Mlawa amesema majibu ya changamoto za mkoa wa Tanga ni maneno magumu ya sayansi yasiyokuwa na alama hivyo wameshauri walimu kuandaa klabu ya somo la sayansi, kuandika maneno magumu hasa masomo ya sayansi na kuwaalika wadau wao CHAVITA ili watoe lugha ya alama.
"Kuimarisha na kukuza lugha ya alama kwa wadau CHAVITA lakini pia pamoja na UWAVIKA kutaimarisha pia mipango ya kuandaa klabu ya (LA) yaani lugha ya alama pekee kwa wadau wote ambao watachangia gharama kidogo kwenye klabu hiyo ambao ni Wazazi/Qalezi, Walimu, Wanahabari, Ustawi wa Jamii, Wahudumu wa Afya, Mahakama na Polisi" alifafanua Mlawa.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments