Na Muhidin Amri,Songea
MKUU wa wilaya ya Songea, amekabidhi vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5 ili kukamilisha ujenzi wa matundu ya choo na vyumba vya madarasa katika Halmashauri mbili za Madaba na Manispaa ya Songea.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni mifuko 260 ya saruji, na bati 30 ambazo zinakwenda kumaliza changamoto ya miundombinu ya elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo kwa watendaji kata Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema amesema, ofisi yake kila mwaka ina kawaida ya kuunga mkono juhudi za wananchi pale ambapo kuna miradi ya maendeleo inayotekelezwa hususani katika sekta ya elimu na afya.
Amesema, lengo la kutoa vifaa hivyo ni kusaidia na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi ambao wanashirikiana na Serikali za vijiji na kata ili wanafunzi katika maeneo hayo wapate sehemu salama na nzuri kwa ajili ya kujisomea.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya,baada ya hapo ofisi yake itafuatilia ili kuona kama msaada huo umefika na umetumika kama ilivyokusudiwa na wataendelea kuunga mkono juhudi za Wananchi wanaojitolea nguvu zao na kwa kuiunga mkono Serikali katika kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao.
Amesema, katika kata ya Mateteleka Halmashauri ya Madaba wanafunzi wanaochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari wanalazimika kutembea umbali wa km 5 kwenda kusoma kata jirani za Mahanje na Wino kutokana na kukosekana kwa shule.
Hata hivyo, kutokana na kero inayowakabili watoto kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule, mwaka jana wameanza ujenzi wa shule ya Sekondari ambapo ofisi ya Mkuu wa wilaya imechangia mifuko 50 ya saruji na Mbunge wa Jimbo Joseph Mhagama ametoa vifaa vya kuezeka na mwaka mwaka ujao shule hiyo itaanza kutumika.
Amesema, kwa sasa wazazi na walezi wanaingia gharama kubwa ya kuwalipia nauli watoto wao na baadhi ya watoto wanalazimika kupanga vyumba uraiani jambo linalosababisha kukutana na changamoto mbalimbali, hivyo mara itakapokamilika wazazi na walezi watapa unafuu wa gharama wanazotumia kwa ajili ya vijana wao.
Mtendaji kata ya Mateteleka Joel Swed, amemshukuru Mkuu wa wilaya kwa msaada huo kwani unakwenda kukamilisha ujenzi wa shule ya Sekondari na hivyo kumaliza kero ya muda mrefu ya watoto wanaotoka katika kata hiyo kwenda kata nyingine kufuata shule.
Kaimu Mtendaji kata ya Seedfarm katika Manispaa ya Songea Jonathan Kambanga amesema, vifaa vilivyotolewa na Mkuu wa wilaya vinakwenda kuongeza nguvu pale ambapo wananchi wameonesha moyo wa kujitolea katika ujenzi wa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa katika kata hiyo.
Kambanga amesema, katika kata ya Seedfarm kuna ujenzi wa Ofisi ya Kata ambao ulianzishwa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali,hata hivyo umeshindwa kukamilika kutokana na ukosefu wa fedha kwa hiyo msada uliotolewa na Mkuu wa wilaya utasaidia sana kuendelea na kazi ya ujenzi.
Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Pololet Mgema kushoto, akikabidhi bati kwa Afisa Mtendaji kata ya Ruvuma Christa Komba katikati ili ziweze kutumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Ruvuma,
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema akimkabidhi kaimu Afisa Mtendaji kata ya Seedfarm katika Manispaa ya Songea Jonathan Kambanga sehemu ya mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Kata.
,Afisa Mtendaji kata ya Mateteleka Halmashauri ya Madaba Joel Swed kulia akipokea mifuko wa saruji kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema ili kukamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata hiyo ulionzishwa na wananchi ili kukabiliana na kero ya wanafunzi wanaotoka katika kata hiyo kwenda kata jirazi za Wino na Mahanje kufuata masomo.
Picha zote na Muhidin Amri.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments