IMEELEZWA kuwa Mafundi Sanifu ni kada muhimu katika maendeleo nchini katika ujenzi wa viwanda na ukuaji wa uchumi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho katika ufunguzi wa kongamano la tatu la mafundi sanifu lililofanyika tarehe 23 Julai 2021 mkoani Dar es Salaam.
Chamuriho amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa mafundi Sanifu katika kufanya kazi na wahandisi na hivyo itaendelea kutoa kipaumbele kwenye vyuo vya VETA na vyuo vya ufundi ili kuhakikisha sera ya viwanda inakuwa endelevu.
"Serikali inatambua mchango wenu na inawekeza kuhakikisha mnapata mafunzi hivyo ni wajibu wenu Mafundi Sanifu kuvitunza viwanda na miundombinu ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuchangia katika pato la taifa" amefafanua Chamuriho.
Aidha, Chamuriho ameongeza kuwa kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) viwango vya uwiano wa kazi za uhandisi ni 1:5:25 ambayo ni kila Mhandisi mmoja anafanya kazi na Mafundi Sanifu 5 na chini yao mafundi stadi 25.
Amesema kuwa kuanzia mwaka 2014 mpaka sasa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) imesajili mafundi sanifu 1,707 kati ya wahitimu 15,260 waliohitimu katika kipindi cha miaka kumi.
"Idadi hiyo ni ndogo hivyo nitoe wito kwa Mafundi Sanifu wote kujisajili kwani ni kosa la kisheria kufanya kazi bila kusajiliwa na bodi na pia kujikosesha haki zenu za msingi" amesema Dkt. Chamuriho
Aidha Chamuriho amewaasa Mafundi Sanifu wote kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na kujiepusha na masuala ya rushwa ili kuisaidia Serikali kufikia azma yake ya kukuza uchumi.
Awali akimkaribisha Waziri huyo, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB Mhandisi Prof. Ninatubu Lema ameiomba Serikali kuhakikisha inaendeleza azma yake ya kuendeleza Mafundi Sanifu katika fani mbalimbali kama matengenezo ya simu, wataalamu wa migodi na wataalamu wa vifaa vya migodi ili kutoa fursa zaidi ya ajira kwa watanzania.
Aidha ameomba Wizara na taasisi za Serikali kutoa kipaumbele kwa wataalamu hawa kwa kuangalia muundo katika ngazi za utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kujali maslahi yao.
Naye Msajili wa Bodi ya Wahandisi Mha Patrick Barozi amesema kuwa bodi inaendelea kusajili, kuendeleza na kudhibiti fani ya uhandisi na hadi Juni 2021 jumla ya wahandisi 31,729 na Mafundi Sanifu 1,707 wamesajiliwa.
Kongamano la tatu la Mafundi Sanifu limehudhuriwa na Mafundi Sanifu zaidi ya 500 kutoka sehemu mbalimbali limebeba kaulimbiu ya Mchango wa Mafundi Sanifu katika maendeleo ya kiteknolojia na ubunifu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments