Watanzania wamlilia mwanamuziki Waziri Ally | ZamotoHabari.


Adeladius Makwega,WHUSM –Dodoma.

MWANAMUZIKI Waziri Ally  Seifu maarufu kama Waziri Njenje amefariki dunia Julai 23,2021 katika Hospitali ya Mwananyamala Jijini Dar es Salaam.

Kulingana  na taarifa zilisombaa katika vyombo mbalimbali vya habari na kuthibitishwa na katibu  Mkuu wa Chama Cha Muziki wa Dansi nchini (CHAMUDATA), Hassani Msumari amesema  ni kweli  mwanamuziki huyo amefariki na msiba upo  nyumbani kwa marehemu  nyuma ya Duka la Dawa la Nakiete Mwenge mwisho Jijini Dar es Salaam.

Kulingana na taarifa zilizokusanywa juu ya mwanamuzi huyo, imefahamika kuwa  aliweza kufanya kazi  ya sanaa ya muziki kwa zaidi ya miaka 50 na miaka 44 pekee hadi anafikwa na umauti amekuwa  ni msanii na kiongozi wa bendi ya The  Kilimanjaro Band.

“Leo ni siku ya Jumamosi kwa desturi yake Waziri Ally alikuwa akiamka asubuhi na kufanya shughuli zake za kawaida na ikifika jioni  anarudi hapa nyumbani kwa mapumziko ili kujiandaa na maonesho yake  ya usiku katika kumbi mbalimbali za  burudani akiwa  na wananjenje-The  Kilimanjaro Band.” Alidokeza Masoud Masoud  ambaye ni Mtangazaji  Mkongwe  wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na mdau mkubwa wa muziki nchini.
 
Sasa hatunaye tena, ndiyo ameondoka, kubwa kwa wanamuziki wa Kitanzania ni kuiga mema ya ndugu yetu Waziri, haswa la kuweza kuwaunganisha  wanamuziki na kuweza kuwafundisha vijana wengi muziki husasani upigaji wa ala  za muziki ameongeza   Masoud Masoud.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mfaume Said, amesema kuwa amepokea kwa masikitiko  msiba huo kwani mchango wa Waziri Ally ni mkubwa na hauna kipimo cha kupimia.

“Kumuenzi ni kuyaiga mazuri yake na kuendelea  kukuza sanaa  ya muziki nchini kwa manufaa  ya kizazi cha leo na kijacho.”Aliongeza  Kaimu Mkurugenzi huyo.

 Mwaanamuziki Waziri Ally ni mzaliwa wa  Pongwe Tanga ataendelea kukumbukwa na wadau wa muziki na Watanzania wengi kwa nyimbo kadha wa kadha kama vile Kinyanyau, Tupendane Mpenzi , Gere na nyingine  nyingi.

…”.  Mie na wangu nyumbani,
        Mambo yangu Burudani,
        Masikio nimeziba,
        Sijali ya mitaani,
      Wangu nimemdhibiti,
      Hasiki wala haoni,
     Jaribuni Kwengine,
      Hapa hamuoni ndani,

Wacha wachawaseme , watasema mchana  ehh  na usiku watalala .”


Kwa  hakika Waziri  Ally  ametutoka , huu ni wakati mgumu kwa  familia, wakati mgumu kwa wapenzi wake wa  muziki na wakati mgumu  kwa  CHAMUDATA na sisi Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulikisikia.” Kwa hakika maneno hayo ya  Kitabu kimojawapo  cha dini yanaufunga ukurasa wa maisha  ya mwanamuziki  Waziri Ally na ni kweli  msiba ni neno gumu, Kwaheri Waziri Ally.


 


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini