Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Kufuatia makadilio ya chini ya uzalishaji wa zao la mahindi wilayani Ludewa mkoani Njombe kuwa tani 17 elfu kwa mwaka huu wananchi wameyaomba mashirika na taasisi mbalimbali kuja kununua mahindi hayo kwa bei itakayo mnufaisha mkulima.
Hayo wameyasema wakati wa mkutano wa mbunge wa jimbo la Ludewa alipofanya ziara katika kijiji cha Itundu kilichopo kata ya Mlangali wilayani humo.
Wananchi hao wamedai kuwa idadi hiyo ya mahindi ni kubwa na wanahofu ya kuharibikiwa na mazao yao kwa kukosa soko kwani shirika la hifadhi ya chakula (NFRA) limekuwa likinunua mahindi hayo kwa kiwango kidogo na kupelekea mazao hayo kubaki kwenye maghara yao.
Costantia Mganwa ni mmoja wa wananchi hao amesema kwa taarifa walizopewa na afisa kilimo wa kata hiyo kuwa NFRA tayari wamekwisha kufika kwaajili ya ununuzi wa mahindi japo bado hawajatoa bei elekezi hivyo wamemuomba mbunge huyo kuwasaidia kuzungumza nao ili wanunue kwa bei nzuri sambamba na kuchukua tani nyingi.
" Kwa mujibu wa afisa wetu wa kilimo hapa Mlangali kwa kata hii pekee tunakadiliwa kuwa na mahindi tani zisizopungua 2500 halafu utakuta NFRA wakija wananunua tani 500 hadi 1000 tani nyingine tunabaki nazo sasa hizi sisi tuzipeke wapi? Tukiyauza reja reja tunayauza kwa bei ya hasara na mengine yanaishia kuoza", Alisema Mganwa.
Kwa upande wa Nicodem Mtweve ambaye naye ni mkulima wa zao hilo amewaomba NFRA kuwalipa fedha kwa wakati kwani wamekuwa wakichukua mahindi halafu pesa hawalipwi kwa muda muafaka kitu ambacho kinawafanya washindwe kutatua matatizo yao kwa wakati.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema atahakikisha wananufaika na kilimo wanachokifanya hivyo tayari ameanza harakati za kuwatafutia masoko.
Amesema ameongea na mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Mhagama na wamekubaliana kushirikiana kwa pamoja kutafuta masoko kwani hata wakulima wa Madaba wanakabiliwa na tatizo hilo la masoko.
Amesema pia bado anaendelea na mazungumzo na shirika la mazao mchanganyiko ili waweze kuja kununua mahindi na kutokana kuwa NFRA huweka kituo Mlangali na Ludewa endapo watafikia makubaliano wataweka kituo katika kijiji cha Amani kata ya Mundindi.
"Safari hii hatutokubali kuona mahindi ya mwananchi yeyote yanaharibika hivyo wananchi wangu naomba tushirikiane kwa pamoja ili kuhakikisha kilimo tulichokifanya kinatuletea manufaa na kutupa nguvu ya kuendelea na kilimo hiki", Alisema Kamonga.
Diwani wa kata ya Mlangali Hamis Kayombo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mlangali ndani(Hawapo pichani) katika mkutano wa mbunge wa kusikiliza changamoto za wananchi.
Wananchi wa kijiji cha Itundu wakifuatilia mkutano wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga baada ya kufanya ziara ya kusikiliza changamoto mbalimbali za wakazi wa kijiji hicho.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akizungumza na wananchi wa Mlangali ndani (hawapo pichani).
Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi wilaya ya Ludewa akiongea na wananchi wa kijiji cha Itundu (hawapo pichani)
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akiongea na wananchi wa kijiji cha Itundu kata ya Mlangali alipofanya ziara ya kusikiliza changamoto za wananchi Kijijini hapo.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mlangali ndani.
Moja ya shamba la mahindi ambalo lipo tayari kwa kuvunwa na kuingizwa sokoni
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments