KIFO CHA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA ELIAS KWANDIKWA CHAWASHTUA CCM, WAMLILIA,WATOA POLE | ZamotoHabari.

Na Mwandishi, Michuzi TV
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias John Kwandikwa ambaye amefariki dunia Agosti 2,2021.

Kwandikwa alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mkoani Dar es Salaam hadi kifo kilimpomkuta.

Taarifa ya CCM iliyotolewa leo Agosti 3,2021 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Shaka Hamdu Shaka amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mbunge wao wa Ushetu.

Katika taarifa hiyo imesema kwamba Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa kwake kwani wamempoteza mtu muhimu aliyekuwa na mchango mkubwa kwa CCM na Utumishi wa Umma.

“Tumepoteza mwanachama wa CCM na mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautosahaulika, alikuwa ni kiongozi shupavu na makini aliyetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria na Utaratibu."

Elias John Kwandikwa, amekuwa Mjumbe wa kamati ya siasa katika wilaya za Kibaha Mjini 2012-2015, Kahama 2015 mpaka sasa na Mjumbe wa halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanga 2015 na Mbunge wa jimbo la Ushetu toka 2015-2021, Aidha amekuwa Naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 2017-2020 na Waziri wa Ulizi na Jeshi la kujenga Taifa hadi umauti unamfika.

Chama Cha Mapinduzi(CCM) kinatoa pole na kuwaombea subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa mpendwa wao familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Ushetu, Ndugu, Jamaa, Marafiki na wote walioguswa na msiba huu.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini