Na Muhidin Amri,Tunduru
MDAU mkubwa wa michezo hapa nchini ambaye ni Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma Hassan Kungu, ametoa mipira 96 yenye thamani ya Sh milioni 4.8 kwa kata zote 24 zilizopo katika jimbo hilo.
Kungu amesema, lengo la kutoa mipira ni moja kati ya jitihada na mikakati yake katika kuibua vipaji na kuendeleza michezo kwa vijana wa Jimbo la Tunduru Kaskazini na wilaya ya Tunduru.
Amesema, katika wilaya ya Tunduru yenye majimbo mawili ya Tunduru Kaskazini na Kusini kuna vijana wengi wenye vipaji vya kucheza mpira wa miguu,hata hivyo baadhi yao hawajapata fursa ya kuonekana kutokana na changamoto ya vifaa ikiwemo mipira jambo linalosababisha kushindwa kutumia na kuonyesha vipaji vyao.
“sasa hivi mpira unalipa sana kwani sio burudani pekee yake,bali ni afya na ajira ambayo imesaidia vijana wengi wa Kitanzania akiwemo Mbwana Samatta anayecheza mpira wa kulipwa nchini Uturuki,hivyo natumaini mipira hii inakwenda kusaidia kuibua vipaji vya vijana katika jimbo la Tunduru”amesema Kungu.
Kungu ambaye pia Mwenyekiti wa Timu ya Namungo Fc inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara amesema,moja ya ahadi zake wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa vijana ni kuendeleza suala la michezo ambalo linaonekana limekosa msukumo sio kwa Serikali tu bali hata kwa wadau licha ya wilaya hiyo kuwa na vijana wengi wenye vipaji.
Amesema,katika miaka mitano kama Mbunge atahakikisha suala la michezo analipa kipaumbele ili kutoa nafasi kwa vijana wengi kuonyesha vipaji vyao na hatimaye kupata nafasi ya kusajiliwa katika Timu mbalimbali za Ligi Daraja la kwanza na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa upande wake Katibu wa madiwani wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Daud Amlima, amemshukuru Mbunge kwa kutoa mipira hiyo kwani inakwenda kuinua sekta ya michezo katika kata zote za Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Amesema, atahakikisha mipira hiyo inafika kwa walengwa na vijana wanaitumia kuendeleza vipaji vyao na kuwasaidia kuondokana na umaskini.
Amesema,kupitia mipira hiyo vijana wanakwenda kupata ajira na wilaya ya Tunduru inakwenda kutangazwa kupitia sekta ya michezo hapa nchini.
Mmoja wa vijana aliyekabidhiwa mipira Haji Rajabu amesema,kama vijana watakwenda kuitumia mipira hiyo kuendeleza vipaji na kuepuka vitendo visivyofaa katika jamiii.
Mbunge wa Jimbo la Tundu ru Kaskazini, Hassan Kungu kushoto akimpa mipira Katibu wa Madiwani Daud Amlima ili kuigawa katika kata zote kwenye jimbo hilo kama mkakati wa kuibua vipaji na kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana.
Picha na Muhidin Amri.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments