KUNA nidhamu ambayo watu wa kundi flani waliamua kujijengea wakiwa waoga wa kueleza ukweli hata wakiona mkubwa wao amefika sehemu ambayo sio sahihi na hakutakiwa kufanya kitu cha aina ambayo amekifanya.
Nidhamu hii ya woga wakati mwingine husababishwa na mambo mengi. Inaweza kuwa umri mdogo, kukosa kipato lakini wakati mwingine akili tu ya wasiwasi, huwafanya watu kushindwa kuchukua majukumu yao ya kukumbushana.
Sio kwamba mkubwa au tajiri hakosei. Anakosea sana tu kwa kuwa na yeye pia ni mwanadamu. Anafanya makosa kama anavyofanya mtu wa umri mdogo, masikini au mtu mwingine yeyote.
Wakati mwingine kitu muhimu hapa ni kujua ni jinsi gani unaweza kumwambia aliye juu yako amefanya kosa na alitakiwa afanye lipi au aseme kipi ukitumia busara nzuri.
Wiki chache zilizopita aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliondolewa katika nafasi yake ndani ya klabu hiyo na kuridishwa mtu makini nimuonavyo mimi, Ezekiel Kamwaga, uamuzi ambao ulifanywa na bodi ya klabu hiyo.
Hakuna mtu ambaye anaweza asimjue Manara kwamba auache uamuzi huo wa bodi ya Simba upite kimyakimya kwake, yaani asijibu kitu hasa ukizingatia kwamba kabla ya uamuzi huo lilipita tukio la kumshambulia aliyekuwa bosi wake Barbara Gonzalez kupitia sauti ya simu.
Baada ya uamuzi huo kama kawaida Manara alijibu mapigo akiishambulia Simba hasa baadhi ya viongozi wake kwa mambo mengi ambayo aliyaona hayakuwa sawa katika kuondolewa kwake.
Hutegemei klabu kama Simba eti ingeweza kukaa chini na kuamua kujibu mashambulizi ya Manara. Wakati mwingine kukaa kimya nako ni jibu tosha na ulikuwa ni uamuzi mzuri na hapa niliungana na MO kwamba hakuna mtu mkubwa kuliko Simba.
Hata hivyo, joto hilo la Manara kumbe lilikuwa zito na MO akajikuta anamshambulia kiungo wake Clatous Chama katika mtandao wa kijamii wa Instagram. Hili lilishangaza wengi kwani hapa bwana mkubwa alifanya makosa hasa kwa kueleza yale katika mitandao.
Niliwahi kuhisi kwamba sidhani kama ni sahihi kwa MO jinsi anavyotumia mitandao ya kijamii wakati mwingine kueleza vitu ambavyo kwa nafasi yake hakutakiwa kufanya hivyo na pengine kuwaachia watu wa chini yake wavifanye.
Kuna namna ambavyo MO sasa anatakiwa kubadilika na kubadili ushiriki wake katika mitandao ya kijamii katika kufubaza hadhi na heshima yake kwa umma ambao unamheshimu kuwa mfano kwa wengine.
MO anatakiwa kutambua kwamba wako ambao wanajifunza mambo kupitia yale anayoyafanya na kwa muamko wa sayansi na teknolojia, wako ambao sasa wanajiunga kwa wingi katika matumizi ya mitandao hii na wanapokutana na vitu kama hivi ni rahisi kuviiga.
Binadamu anafanya makosa na hata MO anaweza kufanya makosa. Walio karibu na kiongozi huyu wanatakiwa kumshauri mambo ya kubadilika sasa katika yale ambayo anayafanya bila kujali kwamba ni uhuru wake.
Wengi wamekuwa wakivutiwa na maisha ya familia ya kitajiri ya Yusuf Bakhresa licha ya ukwasi walionao lakini maisha yao yamekuwa mbali na mitandao. Huu tunaweza kuutumia kama mfano kujifunza lakini pia ukampa elimu fulani ya kujifunza MO.
Kauli ambayo MO aliitumia kwa Chama haikuwa sawa kwani mchezaji huyo ni muajiriwa wa Simba hata kama fedha zilizotoka zilitolewa na yeye kama mwekezaji wakati mwingine kauli za namna hii zinaweza kuchukuliwa kama njia ya kuwafunga midomo watu kuwa huru kuchagua marafiki zao na kuongea kwa uhuru na marafiki zao.
Hili ni lazima tuliseme na ikiwezekana kumshauri MO sasa kubadilika kidogo na kama ataamua kujifanyia tathimini atagundua haraka kwamba kuna eneo alivuka mipaka na sasa anatakiwa kurudi nyuma na kutafuta mwendo mpya ili aweze kuitunza heshima yake.
Hatutakiwi kuogopa kumkumbusha MO katika hili la kutunza nidhamu yake. Tutakuwa hatumtendei haki. Na maisha ili yaende lazima kama binadamu tuwe na nafasi ya kukumbushana tukizingatia kwamba mitandao hii huangaliwa na wengi hata huko mataifa ambayo wanamchukulia MO kama mfanyabiashara mkubwa anayeheshimika. Tusimuache akazidi kupotea litatuharibia wengi na taifa kwa ujumla.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments