Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge akikabidhi cheti kwa washiriki wa bonanza lililotayarishwa na shirika lisilo la kiserikali, Jambo For Development lililofanyika hivi karibuni katika Manispaa ya Bukoba.
Na Mwandishi wetu, Bukoba
ZAIDI ya wanafunzi wa shule za msingi 80,000 wanatarajiwa kufaidika na miradi inayolenga kuboresha shule zao katika wilaya nane za mkoa wa Kagera kufikia mwisho wa mwaka 2022. Wilaya husika ni pamoja na Muleba, Misenyi, Bukoba Manispaa, Karagwe, Biharamulo, Kyerwa, Bukoba DC na Ngara.
Miradi hiyo yenye thamani ya TZS Bilioni 2.9 inaendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Jambo For Development lenye makao yake makuu mkoani Kagera kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania na mdau kutoka nchini Ujerumani, Jambo Bukoba e.V.
Afisa Habari wa Jambo For Development, Lameck Kiula amesema mjini Bukoba hivi karibuni kuwa miradi hiyo inalenga kujenga uwezo kwa waalimu katika wilaya hizo, ujuzi kwa wanafunzi kupitia michezo (Bonanza) na kujenga miundombinu kama madarasa na vyoo vitakavyokuwa na chumba maalumu kuhudumia wasichana walio kwenye hedhi.
Jambo For Development hutumia michezo kama nyenzo ya kuwaleta wadau mbalimbali pamoja na kushirikiana kuboresha elimu, afya na usawa wa kijinsia.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya bonanza lililojumuisha shule nane za msingi kutoka wilaya nane iliyofanyika katika Manispaa ya Bukoba hivi karibuni, Bw. Kiula alisema michezo imekuwa ni njia yenye ufanisi mkubwa sana katika kuongelea mambo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakifumbiwa macho kuongelewa kwa njia za wazi miongoni mwa jamii kama usawa wa kijinsia, maambukizi na ugonjwa wa ukimwi na hedhi.
“Tumekuwa tukifanya kazi na serikali na wafadhili katika kusaidia mradi huu wa kujenga ujuzi kupitia michezo,” alisema.
Kila shule iliyoshiriki michezo hiyo ya bonanza ya wiki iliyopita itapokea jumla TZS Milioni 46 ambazo zitatumika kuimarisha mazingira na miundombinu ya shule hizo. Katika jumla ya TZS Milioni 368 zitakazowekezwa, asilimia 60 itatoka Jambo for Development, asilimia 30 serikalini na asilimia 10 itatoka kwa wananchi. Wastani wa wanafunzi 600 wanatarajiwa kufaidika na miradi hiyo.
Shule za msingi nane zinazotarajiwa kufaidika na wilaya zilipo kwenye mabano ni Rulongo (Muleba), Ndwanilo (Misenyi), Kashai (Bukoba Manispaa), Kabale (Karagwe), Nyakanazi (Biharamulo), Rwensinga (Kyerwa), Kyembale (Bukoba DC) na Mubinyange (Ngara).
“Utaratibu huu wa ushirikiano unaimarisha miradi na kuifanya kuwa endelevu,” alisema Bw. Kiula.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments