NANI ALITUNGA WIMBO WA MALAIKA? ( I ) | ZamotoHabari

Adeladius Makwega.DODOMA

Japokuwa mirabaha na haki ya wimbo huu zinaekezwa mno kwa Fadhili William, huku kumekuwa wasanii kadhaa wakidai kuwa wao ndiyo walioutunga wimbo maarufu wa Malaika.

Wimbo huu kwa miaka zaidi 80 ukiaminika kuwa ulitungwa na kurekodiwa katika mataifa ya Kenya na Tanzania huku ukiwa ni wimbo pekee wenye sumaku kali ya kuitambulisha Afrika ya Mashariki na lugha ya kiswahili.

Malaika ni wimbo unaozungumzia maudhui ya mapenzi ambapo kijana mmoja mdogo anashindwa kumuoa binti mmoja mrembo kwa kuwa hana mali. Kama waswahili wasemavyo mkono mtupu haulambwi.

Kwa miaka hiyo 80 wimbo huu umeweza kurekodiwa katika matoleo mbalimbali na wanamuziki wa kila aina kwani nguvu hiyo ya usumaku ya kupendwa karibu mataifa mengi imekuwa bado ikiendelea kuwavutia wasanii wengi na wapenzi na wanamuziki wengi dunia kuurudia kila uchao.

Kutokana na umaarufu wa wimbo huu neno malaika sasa limekuwa pia neno lenye maana nyingi; kiumbe wa kiroho anayekuwa na umbo la kibinadamu, mjumbe wa Mungu, mlinzi wa binadamu asiyeonekana, mtoto mchanga, pia ni wingi wa neno laika, mwisho ni MWANAMKE MPOLE, MNYENYEKEVU, MWENYE UMBO & SURA NZURI.

Maana hii ya mwisho ya neno LAIKA/MALAIKA ya MWANAMKE MPOLE, MNYENYEKEVU, MWENYE UMBO & SURA NZURI ndiyo iliyokuja baada ya kutumiwa katika wimbo huo kwa miaka zaidi ya 80 katika lugha ya Kiswahili.

Fadhili William ambaye alikuwa mwanamuziki wa Kenya anahusishwa na wimbo huo kutokana na yeye kuwa mtu wa kwanza wa kuurecodi wimbo huo studio na kusaidia kufahamika zaidi na kuchezwa katika kumbi za muziki na redio nyingi Afrika ya Mashariki.

Ndugu William kila mara alikuwa akisisitiza kuwa wimbo huo ni wake huku akieleza namna alivyoweza kuutunga hadi kuurekodi mwaka 1960 na  bendi yake ya Jambo  Boys.


William ambaye ni ni Mkenya huku akiungwa mkono na Wakenya wengi kuwa ndiye mwenye haki na wimbo huo alizaliwa Novemba 11, 1938 kama Fadhili William Mdawida na aliwahi kusimulia namna alivyotunga kibao hicho.


“Nilikuwa na mpenzi wangu aliyekuwa mrembo sana akifahamika kama Fanny na kwa urembo wake nilimpa jina Malaika lakini ilipofika wakati wa kumchumbia binti huyo, nilikosa pesa za mahari kwa kuwa nilikuwa fukara mno, huku baba yangu alifariki wakati nikiwa na miaka miwili tu. Umasikini wetu ulifanya Fanny akaolewa na jamaa mwingine tajiri. Ili kupoza maumivuhayo nilimtungia wimbo huu huku mumewe Fanny akiusikiliza katika redio bila ya kujua maana ya fumbo hilo, kumbe malaika ndiye mkewe na mchumba wangu wa zamani.”


Hayo ya Fadhili William ni pale ninapogubika upande wa kwanza wa shilingi. Je kuna nini zaidi katika wimbo huu? Subiri matini ijayo.

 

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 



Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini