TaSUBa yahimizwa kuwa ya kimataifa | ZamotoHabari


Na. John Mapepele

Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Saidi Yakubu ameutaka uongozi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kuifanya taasisi hiyo kuwa kituo chenye hadhi ya kimataifa kwenye utoaji wa taaluma  ya Sanaa na utamaduni kuliko ilivyo sasa

Yakubu amesema hayo leo Februari 7, 2022 alipofanya ziara chuoni hapo na kuongea na watumishi  na Menejimenti ya TaSUBa na baadaye kukagua shughuli mbalimbali  zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

Amefafanua kuwa kutokana na upekee wa taaluma zinazotolewa na chuo hicho ambazo zinaendana  na vyuo vya kimataifa hakuna sababu ya chuo hicho kubaki na hadhi yake ya sasa inayoongozwa na dira ya kutoa taaluma katika ubora kwa ngazi ya Afrika.

" Ni wazi kwamba  kwa upekee wa chuo chetu na kozi zinazotolewa hapa ni lazima tuondokane na  na fikra za Bagamoyo, Tanzania au hadhi ya Afrika na badala yake tuwe wa kimataifa " ameongeza Yakubu.

Ameutaka uongozi kuwa mbunifu kwa kutumia raslimali za wizara mama kujitanua  zaidi nchi nzima badala ya kufikiria  eneo la Bagamoyo pekee.

Amekitaka chuo kuongeza udahili wa wanachuo ili hadhi ya chuo hicho iwe ya kimataifa ambapo amesisitiza  kuwachukua pia wanafunzi kutoka nje ya Tanzania ili wawe mabalozi wa kukitangaza chuo katika nchi zao.





 
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini