SIMBA SC YATUA BENIN NA MALENGO YAKE YA KUFUZU ROBO FAINALI UGENINI | ZamotoHabari


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Kikosi cha timu ya Simba SC kimetua mjini Cotonou nchini Benin kujiandaa na mchezo wake wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya wenyeji wa hapo, Asec Mimosas ya Ivory Coast mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Stade de l'Amitie siku ya Jumapili, Machi 20, 2022.

Akizungumza na Michuzi TV baada ya kutua nchini humo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally amesema wametua nchini Benin majira ya saa 6 mchana, sawa na saa 8 mchana kwa saa za Afrika Mashariki huku wakiwa na lengo kubwa la kufuzu hatua inayofuata wakiwa katika ardhi ya ugenini.

Ahmed amesema tangu wametua nchini Benin wameona hali ya hewa ni sanjari na sehemu walipotoa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, hali ya joto, hali hiyo inasababishwa na nchi hiyo ya Benin kupakana na Bahari.

“Tangu tumefika hapa Benin tumeona kuna hali ya joto kama nyumbani Dar es Salaam, tuliposhuka pale Uwanja wa Ndege, Wachezaji walikuwa wamevaa Makoti lakini baada ya kushuka kwenye Ndege kila mtu alionekana anavua Koti lake kwa sababu ya Joto”, amesema Ahmed.

Amesema tangu wametua Uwanja wa Ndege wamepata mapokezi mazuri kutoka kwa Watanzania wachache waliofika uwanjani hapo kwa ajili ya kuilaki timu hiyo, amesema hakuna shamra shamra nyingi kutoka kwa wenyeji kutokana na wao (Asec Mimosas) kuwa ugenini pia.

“Tumepata mapokezi ya Watanzania wachache ambao wapo hapa nchini Benin, lakini hatukuona fujo wala kelele kutokana na wapinzani wetu na wao kuwa ugenini kama sisi “, ameeleza Ahmed

Kuhusu ratiba kuelekea mchezo huo wa siku ya Jumapili, amesema timu ina malengo makubwa ya kupata ushindi kwenye mchezo huo, huku akieleza Wachezaji na Benchi la Ufundi la timu hiyo wakiwa na molari ya hali ya juu kufuzu hatua inayofuata wakiwa ugenini.

Ahmed ameongeza, “Asec Mimosas wapo hapa kwa muda mrefu na wameshinda michezo yao miwili wakiwa hapa hapa Benin, wamewafunga RS Berkane wamewafunga pia USGN wakiwa hapa hapa, sisi tutaingia kwa tahadhari kubwa ili tusipoteze mchezo huo”.

Hadi sasa, Simba SC wanaongoza Kundi D la Michuano hiyo wakiwa na alama 7 wakati Asec Mimosas wakifungana alama na RS Berkane wote wakiwa na alama 6 huku USGN ya Niger wakiburuza mkia wakiwa na alama 4 pekee.










Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini