MCHENGERWA-WASHINDI WA TUZO ZA MUZIKI WAANZA KUSAJILIWA NSSF NA NHIF. | ZamotoHabari



Na John Mapepele

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imeanza kutekeleza ahadi ilizotoa kwa washindi wote wa Tuzo za Muziki (TMA 2021) wakati wa kilele cha usiku wa utoaji wa Tuzo hizo Aprili 2, 2022 ili kuinua na kuboresha maisha yao zimeanza kutekelezwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa leo, Aprili 24, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo amesema washindi wa Tuzo za Muziki tayari wameshafanyiwa semina kuhusu BIMA ya Afya na jinsi ya kujisajili kwenye Mfuko wa Penseni na makampuni yanayohusika kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili waweze kuzitambua vema huduma hizo za BIMA ya Afya na Mfuko wa Pensheni.

Aidha Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya tuzo za Muziki nchini, Serikali mbali na kutoa tuzo na fedha taslim kwa washindi wote pia ilitoa zawadi ya kuwakatia BIMA ya Afya washindi wote wa Tuzo za mwaka huu kwa mwaka mzima ili kuwaondolea kadhia ya kupata matibabu wakiwa katika shughuli zao za Muziki na pia kuwasajili katika mfuko wa pensheni Wasanii wote washindi wa Tuzo hizo (TMA 2021) na kuwalipia mwaka mzima ikiwa ni mwanzo wa kuwaanzishia mfumo wa kujiwekea akiba ya uzeeni.

Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea kutoa zawadi kubwa ambazo zitaamsha ari ya wasanii kushindana zaidi kitu ambacho kitachochea ubunifu wa kufanya kazi bofra ambazo watafaidika nazo.

“Sisi kama Serikali tumejipanga kuona namna bora ya kuwasaidia wasanii wetu hata kama ikiwa ni kuwazawadia makazi tutafanya nia ni kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao’ amesisitiza Mchengerwa

Akifungua kikao cha Wasanii walioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA 2021) kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Matiko Mniko alisema kikao hicho ni kwaajili ya kutoa semina na kuanza kuwasajili wasanii hao katika Mifuko ya NSSF na NHIF.

Mniko aliwapongeza Washindi wa TMA 2021 kwa kuitikia wito wa kushiriki Semina hiyo ya mafuzo yanayohusu BIMA ya Afya na mafao ya Pensheni kwa manufaa yao ya baadae kutokana na kazi zao za Sanaa.

Kwa upande wa waendesha semina kwa Wasanii wa TMA 2021 wamepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Sanaa hapa nchini.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF Bi.Lulu Mengele amesema NSSF itaendelea kushirikiana na Serikali katika safari ya kufanya mapinduzi kwenye sekta ya Sanaa, naye Meneja wa NHIF Mkoa-Ilala Bw. Evance Nyangasa aliipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika kuwatengenezea mazingira mazuri Wasanii ya kutekeleza Kazi zao za Sanaa.

Nay mshindi wa Tuzo hizo katika kipengele Cha Taarab Mzee Yusuph kwa niaba ya washiriki wenzake aliishukuru Serikali ya awamu ya sita (6) chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyowajali Wasanii, wanamichezo na Wadau wa Sanaa kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Kwa kusema ukweli tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutujali sisi wasanii, tunaahidi kuendelea kuboresha kazi zetu ili tuweze kupata masoko ya kimataifa.




Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini