SIMBA SC YAPATA USHINDI WA BAO 1-0 DHIDI YA ORLANDO PIRATES FC | ZamotoHabari


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

SIMBA SC wameondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates FC katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, kwenye mchezo uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Bao pekee la Simba SC limefungwa na Beki wa pembeni Shomari Kapombe dakika ya 68 kwa mkwaju wa Penalti baada ya Mshambuliaji wa timu hiyo, Bernard Morrison kuangushwa kwenye eneo la boksi. Licha ya bao hilo, Simba SC waliumudu na kuutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa katika dakika zote 90.

Bao hilo la Kapombe linaipa uongozi Simba SC katika mchezo wa mkondo wa kwanza, ambapo Aprili 24, 2022 itaenda Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa pili wa hatua hiyo ya Robo Fainali, Wekundu wa Msimbazi watalazimika kuulinda ushindi huo kuhakikisha hawaruhusu bao ili kutinga Nusu Fainali ya Mashindano hayo.

Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na Mashabiki lukuki takribani Elfu 60 (60,000) wa Simba SC, Wanamsimbazi walianza na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Henock Inonga, Serge Pascal Wawa, Jonas Mkude, Pape Sakho, Taddeo Lwanga, Chris Mugalu, Bernard Morrison, Peter Banda. Baadae kipindi cha pili waliingia, Muzamiru Yassin, Kibu Dennis, Rally Bwalya, Kagere na Yusuph Mhilu.

Kikosi cha Orlando Pirates FC kilianza na Richard Ofari, Happy Jele, Nyauza, Protus Ndlovu, Daniel Hotto, Thabang Monare, Kabelo Dlamini, Goodman Mosele, Kwane Peprah, Innocent Maela, Bandile Shandu.


 

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini