UKUBWA WA TIMU SIMBA NA MWAMUZI KUTOANGALIA VAR...WENGINE CHEFUU | ZamotoHabari



Na Said Mwishehe, Michuzi TV

JUZI kati hapa yaani Aprili 17 mwaka huu tumeshuhudia mpira mkubwa ukichezwa katika Uwanja wa Mkapa uliopo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.Ndio uwanja Temeke na Mkoa ni Dar es Salaam.Ndio nafahamu zamani Dar es Salaam lilikuwa Jiji lakini yalifanyika mabadiliko hivyo ni mkoa kama mikoa mingine.

Mchezo uliochezwa siku hiyo ulihusisha timu ya Simba Sports Club dhidi ya timu ya soka ya Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini.

Katika Mchezo ule Simba walikuwa nyumbani na kama unavyojuaga wenyewe wanamsemo wao kwamba kwa 'MKAPA HATOKI MTU' .Na ndio ukweli Orlando hakutoka, alikufa kwa kupigwa goli moja, hajatoka, kama Simba wanasema hatoki mtu wao wanatokaje?

Unashangaa kufungwa Orlando kwa Mkapa? Acha mambo yako wewe .Wamekufa wengi tu, waulize Al Ahly walikuja kwa Mkapa na wakafa, Simba ndio Simba.

Basi bwana katika ule mchezo wa Simba na Orlando kama nilivyosema mpira uliochezwa ulikuwa mkubwa sana, ninaposema ulikuwa mkubwa watu wa Soka wananielewa.Hata hivyo pamoja na uwezo mkubwa wa wachezaji wa Orlando lakini mbele ya Simba walionekana wa kawaida sana.Umiliki wa mpira kwa dakika zote 90 Simba waliongoza, ndivyo takwimu zinavyoonesha.

Nikiri kwa Simba walikofikia katika mechi za Kimataifa wanaostahili pongezi, sifa na kupigiwa makofi.Hakika Simba wanaliheshimisha soka la Tanzania na soka la Afrika Mashariki.

Wanashiriki mashindano ya Kimataifa kwa mwaka wa nne mfululizo,tena kwa wakifika katika hatua nzuri.Hongereni Simba, hongereni wachezaji na benchi la ufundi, hongera kwa mwekezaji, anajua anakotaka Simba ifike.

Hongera kwa Madaam CEO Babra Gonzalez. Mama unajua na siku hizi kuna ule msemo wanaosema unaupiga mwingi, hakika madaam katika soka la Tanzania na Afrika unaupiga mwingi sana.Unajua kutumia vema akili yako.

Ngoja niachane na hizi mambo za kutoa hongera Kuna watu wanachukia, hawataki kuona Simba wanapewa hongera kwa mafanikio yao .Lakini tujiulize hivi kweli kwa Simba ilikofikia haistahili kusifiwa? Haistahili pongezi? Chefuuuuu

Unahitaji kuwa na roho ya kichawi kubishana na ukweli.Simba imepiga hatua, tena hatua kubwa sana. Hongereni Simba hata kama wengine wananuna.

Ngoja nirudi kwenye hoja yangu iliyonisukuma kuandika haya maelezo. Unajua nini mtu wangu!Katika mechi ya Simba na Orlando pamoja na kuwapo kwa mwamuzi wa kati na wasaidizi wake bado kullikuwa na VAR.

Nikiri tu ni kwa mara ya kwanza VAR kufungwa katika ardhi ya Tanzania, ndio mara ya kwanza kufungwa katika Uwanja wa Mkapa. Kupitia Simba tumeshuhudia soka la Tanzania linaandika historia kubwa ambayo haitafutika.Ndio VAR imetumika Kwa mara ya kwanza kuangalia maamuzi ya chezo wa Simba na Orlando.

Hapo ndipo Simba wametufikisha.Ukitaka timu yako nayo itumie VAR Kuna hatua unatakiwa kuifikia kinyume na hapo utasikia na kuona kwa timu kubwa tu zinapocheza mechi kubwa.

Sasa bwana iko hivi VAR baada ya kufungwa katika Uwanja wa Mkapa wapo wenzangu na mimi wamebakia na malalamiko oooh mbona VAR haikutumika katika kusaidia kutoa maamuzi kwenye mchezo ule wa Simba na Orlando? Tena wanaotoa madai hayo wanasema maneno mengi mengi.

Wengine wanasema VAR ilizimwa na hivyo haikuwa ikifanya kazi.Wengine tena wanasema ilikuwa imewashwa lakini kwanini muamuzi hakwenda kujiridhisha na maamuzi ya ile penalty aliyoitoa kwa Simba baada ya Bernard Morrison kuchezewa rafu ndani ya 18.

Na Shomari Kapombe hakufanya ajizi ,aliipiga utamu penati na kuingia nyavuni.Kuna ndugu yangu mmoja anaitwa Hamis anafanya shughuli zake za Saluni pale Banana kwenda njia ya sekondari ya Air Wingi,tumebishana sana kuhusu VAR kisa Refa hakwenda kuiangalia.Namheshimu acha nimvumilie ndio ugeni wa VAR.

Pamoja na uwepo wa VAR ambayo kimsingi inayokaa pale uwanjani ni Screen tu ambayo mwamuzi anaweza kwenda kujiridhisha na maamuzi aliyoyatoa kama kunakuwa na utata.Na katika penati ya Simba kabla ya kusema penati alifanya mawasiliano na waliokuwa ndani na wakamwambia kweli ni penati.

Lakini bado mashabiki maandazi wanasema kwanini hakwenda kwenye screen kuangalia? Swali unakwenda kuangalia ya nini wakati ulichoamua kiko sahihi?

Hata hivyo kujifunza sio dhambi na kwa kuwa mjadala mkubwa katika mechi ile ya Simba na Orlando umebakia kwenye VAR nikaona isiwe tabu hebu ngoja niangalie wanaposema VAR wanamaanisha nini? Ni hivi VAR ni kifupi Cha maneno yanayosomeka Video Referee Assistance).

Na hiyo ni teknolojia ambayo imeletwa na chama cha marefa kupitia International Football Association Board (IFAB), ikiwa na lengo la kusahisha refa wa kati katika maamuzi yake kupitia video.

Kutokana na uwepo wa teknolojia hiyo kwa sasa mechi nyingi zinakuwa na waamuzi wanne yaani refa wa kati, wasaidizi wapembeni wawili pamoja na mwamuzi wa akiba, japokuwa kuna baadhi ya michuano kunakuwa na marefa nyuma ya magoli.

Hivyo kutokana na makosa ya kibinadamu chama cha maamuzi wasaidizi waliomba kuwepo kwa refa wa tano ambaye yeye atakaa katika video akiwa na kifaa kwa ajili ya kuwasiliana na refa wa kati. Ndio maana hata katika Mechi ya Simba na Orlando refa kabla ya kutoa penati alifanya mawasiliano.Sote tuliona na kama tuliona shida iko wapi?

Hata hivyo tujikumbushe kidogo baadhi ya mambo ambayo yanaangaliwa kwenye Video Referee Assistance ambayo maarufu tunaita VAR.

Ukweli ni kwamba teknolojia hii ya VAR inaonyesha mapitio ya vitu vinne, moja ni Goli, Penati, Kadi nyekundu na nne ni Kutambua makosa (mistake identity).

Unaweza kuuliza inafanyaje kazi? Ni iko hivi kutofautisha kuna vifupisho nitatumia ili usichanganyikiwe, VAR ni Video referee assistance maaana yake ni ile kamera inayorekodi tukio, wakati AVAR kirefu chake ni Assistant Video Assistance Referee ikiwa na maana kuwa ni yule mtu ambaye anaopareti na VAR na kumuambia refa wa kati

VOR ni Video Operation Room ni chumba maalumu ambacho AVAR anakaa ambapo anakuwa na mtu anaitwa RO huyu ni Replay Operator, hawa wakina AVAR ni refa tu kama wengine so hawezi au ana ufinyu kujua kuhusu na mitambo ya kurusha mpira kwahiyo RO ni anamsaidia kufanya marejeo ya tukio analohitaji kuliona, pia OFR maana yake ni On-field referee mwamuzi wa kati ambaye anachezesha mechi.

Angalau hapo tutakuwa tumepata kitu kidogo lakini nihitimishe kwa kusema hivi kama kweli Simba waliweza kufanya ushawishi wowote ule kwa mfano ili tu VAR isitumike basi tukubaliane Simba ni kubwa sana ,itakuwa kubwa kuliko Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Ndio kama VAR Inaweza kufungwa halafu wao wakawa na nguvu kiasi cha waamuzi kutoitumia Simba lazima itakuwa kubwa sana .Na mwenye kuamini hivyo inabidi awe na akili ambayo imechanganyika na akili ya Pusi a.k.a Nyau.

Ninachoamini mimi Simba ni timu kubwa kwa sasa na CAF wanaitambua kwa ukubwa wake lakini sio kiasi cha kubadilisha maamuzi uwanjani ili kunufaika nayo.

Tujifunze kwa Simba wamewezaje kufika hapo walikofika? Sio dhambi kujifunza kwa Simba , kwa Tanzania unapozungumzia michuano ya Kimataifa unamuona yeye kwanza halafu ndio utafute na wengine kwa nafasi zao.

Na Simba hana roho mbaya tayari amewatafutia nafasi na wenzake yaani timu nne kutoka Tanzania zitashiriki michuano ya Kimataifa.Inatosha kwa leo kama umechukia mwamuzi kutoangalia VAR kanywe sumu ya Panya Urest in Peace.

Halafu Ukisharest napokea rambi rambi kwa namba hii 0713833822 jina litatokea Said Mwishehe na Ukirest kazi yangu itakuwa kuwaambia Watanzania marehemu amekufa kifo cha kujitakia kilichotokana na roho mbaya yake.Inatosha.


 

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini