Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KLABU ya Soka ya Simba imekabidhiwa mfano wa hundi ya Shilingi Milioni 50 na Kampuni ya Michezo ya kubashiri ya Sportpesa ikiwa ni zawadi baada ya kufika Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) msimu wa 2021-2022, fedha hiyo ni sehemu ya bonasi kwa kufika hatua hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya makabidhiano ya mfano wa hundi ya kiasi hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas amesema wamekabidhi zawadi hiyo kwa Simba SC kutokana na matokeo yao uwanjani yanayoridhisha licha ya kujikwaa katika hatua hiyo ya Robo Fainali ya CAF CC.
“Mkataba wetu sisi Sportpesa na Simba SC ambao unaenda kumalizika mwishoni mwa msimu huu, makubaliano wanaposhiriki mashindano ya CAF, iwe Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho barani Afrika na wanapofikia Robo Fainali au zaidi kutakuwa na bonasi sanjari na Ligi yetu ya nyumbani, wanapochukua Ubingwa vile vile kuna bonasi wanapewa”, amesema Tarimba.
“Hadi sasa, Simba SC wamepewa Shilingi Milioni 100/- kila walipokuwa wanachukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika misimu minne waliyotwaa Ubingwa wa Ligi hiyo”, ameongeza Tarimba.
Tarimba amesema wameendelea kutoa fedha za Udhamini kwa mujibu wa mkataba, amesema Simba SC wanastahili kupongezwa kuchukua fedha nyingi za bonasi wanazopata katika mashindano ya Kimataifa wanayoshiriki mara kwa mara.
Tarimba amesema, “Tunafurahi kuona Simba SC inafanikiwa ndani na nje ya mipaka yetu, kwa sababu tunaamini sisi Sportpesa tupo nyuma yao kama Wadhamini wao, katika kipindi cha miaka mitano kulikuwa hakuna msuguano wala mgongano wowote baina ya pande zote mbili”.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez amewashukuru Kampuni ya Sportpesa kutoa kiasi hicho cha fedha (Tsh. Mil 50) kama bonasi ili kuwapa motisha Wachezaji kupambania timu na kufika malengo yake ya kufika mbali katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje.
“Kwa mujibu wa mkataba wa Sportpesa, Simba SC ndio Klabu pekee inaongoza kuchukua bonasi zinazotolewa na Sportpesa baada ya kufanya vizuri katika Michuano mbalimbali, tumechukua bonasi zaidi ya Milioni 500 ndani ya miaka minne kwenye mashindano ya ndani na nje nchi”, amesema Barbara.
Barbara amesema Simba SC inatambua mchango wa Sportpesa katika mkataba wa udhamini, amesema wanaendelea na mazungumzo kuboresha mkataba huo ambao unafika ukingoni, ili kuboresha zaidi mkataba mpya ambao watasaini tena.
“Wametusaidia, wametupa nafasi ya kutosha, leo Simba SC isingepata nafasi ya kucheza na Sevilla FC ya Hispania, jambo la kipekee ni historia, leo tusingepata nafasi ya kuongea na wadau wa Everton, lakini kupitia wao Sportpesa imewezekana”, amesema Barbara.
Kutoka kulia ni Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, wa pili ni Mchezaji wa Klabu hiyo, Erasto Nyoni, wa tatu ni Afisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Sabrina Msuya.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments