KIONGOZI WA MABOHORA DUNIANI ATUA NCHINI KUFANYA ROYAL TOUR TANZANIA | ZamotoHabari






Na John Mapepele,

Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Mabohora (Dawoodi Bohoras); Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin, ametua nchini leo Alhamisi Juni 16, 2022, tayari kufanya ziara ya kiimani na mapumziko mafupi.


Saydna Mufaddal, atakuwa nchini kwa takribani wiki mbili ambapo pamoja na shughuli za kiimani amekuja kuunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza na kuifungua nchi hasa kupitia filamu ya Royal Tour.

“Akiwa nchini amekuja kuunga mkono malengo ya Royal Tour na yeye mwenyewe na wafuasi wake watakwenda mapumziko hapa nchini na msafara wake wote katika maeneo mbalimbali na pia iwapo taratibu zitakamilika na akaridhia anaweza kufanya mhadhara wake mkubwa wa kidini Julai hapa nchini ambapo wafuasi wake kati ya 30,000 hadi 40,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani humfuata na tunajipanga ikitokea hivyo tutawaonesha watu hao na mabohora wengine duniani filamu ya Royal Tour,” alisema mmoja wa viongozi wa dhehebu hilo nchini Bw. Zainuldeen Adamjee.

Akimpokea Kiongozi huyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema amewasilisha kwa kiongozi huyo salaam za Mhe Rais Samia ikiwemo utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mhadhara mkubwa wa mwaka wa kiongozi huyo utakaoleta maelfu ya watu hapa nchini.

“Hii ni sehemu ya muendelezo wa Royal Tour (post royal tour) ambapo Mhe Rais wetu amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu na sasa wawekezaji na watalii wakiwemo viongozi wa kimataifa wa kiimani na wa kijamii nao wanazidi kuja Tanzania. Kwa eneo letu sisi la utamaduni tumemhakikishia Sheikh kuwa Tanzania ni salama na aendelee kutuombea amani lakini pia alete wafuasi wake wengi zaidi kuja kutembelea na kuwekeza Tanzania,” alisema Waziri Mchengerwa.

Katika mapokezi hayo, Waziri Mchengerwa, aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, ambaye pia anasimamia Kamati ya Rais iliyoratibu Royal Tour.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini