Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatetengeneza na kusimamia Sera ya Filamu itakayohakikisha kukua kwa utamaduni na kusaidia kuweka mazingira bora ya uwekezaji utakoimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mengine.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Usiku wa kuamkia leo wakati wa Sherehe za Ufunguzi wa Tamasha la 25 la Filamu kwa Nchi za Jahazi (ZIFF) zilizofanyika katika Ukumbi wa Ngome-Kongwe, Forodhani Jijini hapa.
Amesema kuwa hiyo ni kutokana na uhalisia kwamba mwendelezo wa harakati za Tamasha la Filamu na Maonyesho ya shughuli mbali mbali za Utamaduni wa Asili wa Mzanzibari na Nchi za Jahazi, zinaitambulisha Zanzibar duniani na kwamba ni miongoni ma fursa muhimu za kuikuza Nchi kiuchumi.
Amesema matukio ya kitamaduni, kama vile Tamasha la ZIFF linaloendelea sasa nchini hapa, huwezesha ubadilishanaji wa moja kwa moja wa mawazo, mila, silka na maongezi kati ya jamii za watu tofauti, hasa kwa kuzingatia uzuri na upekee wa Visiwa vya Zanzibar tangu asili uliotokana na historia ndefu katika ulimwengu wa ustaarabu.
Mheshimiwa Othman amebainisha kuwa Binaadamu daima hujisikia vyema anapoweza kutambulisha ustaarabu wake na wengine wakasifia na kuweza kujifunza kutoka kwake, ambapo hiyo ni katika siri za Tamasha la Utamauni wa Nchi za Jahazi.
"Katika kujifunza tunapata kubadilishana mawazo, ujuzi, ufahamu na elimu, vitu ambavyo ni muhimu kwa maendeleo ya binadamu na ni sehemu muhimu sana ya kuenzi na kutukuza utu wetu katika njia ya mshikamano na hivyo kuwa kielelezo cha haki, amani na ustawi wa kimataifa", amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Aidha amesema kuwa filamu zinazungumza lugha moja; ni muhimu na zina maana sawa kwa ulimwengu na watu wote, bila kujali asili zao za kitaifa, kitamaduni au kijamii ambapo pia ni njia moja maarufu ya sanaa za kisasa, zinazovunjavunja vizuizi baina ya watu, mataifa na tamaduni, huku zikisisitiza maadili, hisia na utashi ambao mwanadamu daima anapenda kuudhihirisha kupitia kubadilishana mawazo.
Katika nasaha zake Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wageni ambao ni kutoka ndani na nje ya Afrika, wakiwemo washiriki kutoka Oman, Falme za Kiarabu, na Umoja wa Ulaya, kutenga muda na kutembelea vivutio vya Zanzibar kwa ujumla, na kujionea urithi na utajiri wa utamaduni wa visiwa hivi, huku akisisitiza kwa kusema, "haya ni maendeleo ya kipekee ya Tanzania ya leo na ndipo tunapoona umuhimu wa kuwa na Tamasha la Kimataifa".
Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana, katika Hafla hiyo, na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, amebainisha kuwa ni furaha iliyoje kuona hayo yakitokea Zanzibar, katika Mji Mkongwe, Mji wa Kale, Mji wa Urithi wa Kimataifa, pahala ambapo pia pamekuwa makutano ya binadamu wote kwa zaidi ya karne 5 sasa, miongoni mwao wakitokea Bara Hindi, Bara Arabu, Uchina, Marekani, Ulaya na Afrika yote kupitia njia mbalimbali zikiwemo za biashara na mahusiano mema kwa kipindi cha zaidi ya miaka Mia Tano.
"Kupitia mahusiano haya wakaambukizana utamaduni na urithi wa dunia; ndiyo maana ni furaha kubwa kuona kwamba kwa kupitia Tamasha hili tunaendeleza nguzo hiyo moja muhimu ya utu na urithi wa binadamu", ameongeza Mheshimiwa Othman.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bi Tabia Maulid Mwita amesema kuwa daima amekuwa akifahamisha tija ya ziada iliyopo katika ufanikishaji wa Tamasha la Filamu la ZIFF hapa visiwani, ikiwemo upeo mpya wa ubunifu baina ya watengeneza- filamu wa Tanzania, na kwamba ikitokea shaka yoyote dhidi ya mila na silka za asili, ni vyema watu wasisite kuibuka na kushauri ili kunusuru utamaduni uliojaa ustaarabu wa Kizanzibari.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Bw. Hassan Mitawi amesema kuwa filamu ni chombo muhimu cha kuelezea maisha na utamaduni wa watu na jamii yeyote inayohitaji maendeleo katika nyanja zote za maisha zikiwemo za uchumi.
Akieleza mafanikio ya ZIFF kwa Kpindi cha Miaka 25 tangu kuasisiwa kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha hilo hapa Visiwani, Profesa Martin Mhando amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, tasnia ya filamu ya Tanzania na Afrika kwa ujumla imestawi, ambapo filamu bora zaidi za Kiafrika na hata za Kitanzania zinaonekana katika orodha ya Tuzo za Kimataifa.
Pamoja na hotuba na burudani mbali mbali za kusisimua, zikiwemo Ngoma za Asili za Mwanandege na Bomu kutoka kwa Wasanii wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar(JKU) mbele ya mamia ya washiriki kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, hafla hiyo ilishuhudia Sehemu ya Filamu ya Hadithi mashuhuri visiwani hapa inayotokana na Riwaya ya Mtunzi Shafi Adam Shafi, inayojulikana kwa jina la 'Vuta-N'kuvute' ambayo imeandaliwa na Mtayarishaji Amil Shivji kutoka Dar es Salaam, Tanzania.
Filamu hiyo, pamoja na kuonyesha mazingira ya kihistoria na asili ya Visiwa vya Unguja na Pemba, inasimulia hadithi ya msichana aliyejikuta katika wimbi la kupigania uhuru hapa Zanzibar, ambaye hatimaye aliamua kuchaguwa upande wa haki, kama sehemu ya mafunzo ya mshikamano wa watu wa rika, rangi, imani na tamaduni tofauti katika kusimamia heshima, utu na uhuru wa binaadamu maishani.
Aidha, Watengeneza filamu wa Kitanzania wameelezwa kupitia Tamasha hilo, watapata fursa adhimu ya kutazama filamu kutoka nchi mbalimbali zilizochaguliwa vyema, zenye mandhari na mitindo mbalimbali, ili kujifunza zaidi.
Kwamujibu wa taarifa ya Waandaaji ni kwamba, kwa Mwaka huu takriban filamu 3450 kutoka Nchi 33 ziliingia katika mchujo na hatimaye 101 zitapata fursa ya kuonyeshwa kupitia Tamasha hilo.
Watu Mashuhuri na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Asasi za Kiraia wamejumuika katika Sherehe hiyo, ambao ni pamoja na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui; baadhi ya Mabalozi wa Nchi za Kigeni; Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya ZIFF; Wasanii na Watengeneza Filamu mashuhuri kutoka ndani na Nje ya Afrika; Wakurugenzi na Watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Bw. Khamis Abdulla Said.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments