Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MABINGWA wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Yanga SC wametwaa ubingwa wa Michuano ya ‘Azam Sports Federation Cup’ (ASFC) baada ya ushindi wa mikwaju ya Penalti 4-1 dhidi ya Coastal Union FC ya Tanga iliyokuwa bora zaidi kwenye mchezo huo wa Fainali uliopigwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Katika mchezo huo ulihitimishwa na dakika 120 kwa sare ya bao 3-3, Coastal Union FC walianza kufungua ukurasa wa mabao yake kupitia kwa Mshambuliaji wake, Abdul Suleiman Sopu kwenye dakika ya 11 na kuifanya timu hiyo ya Wagosi wa Kaya kwenda mapumziko wakiwa na uoongozi wa bao 1-0.
Kipindi cha pili, Yanga SC walisawazisha bao hilo kupitia kwa Kiungo Mshambuliaji, Feisal Salum Feitoto dakika 57 ya mchezo. Hata hivyo dakika ya 82, Yanga SC walipata bao la uongozi kupitia kwa Mshambuliaji Heritier Makambo baada na kufanya matokeo kuwa bao 2-1.
Dakika ya 88 Coastal Union FC walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Mshambuliaji wake yule yule, Sopu aliyepiga Kichwa safi kilichomshinda Golikipa wa Yanga SC, Djigui Diarra. Sopu aliipatia tena Coastal Union bao la tatu na la kuongoza dakika ya 98 baada ya kuichachafya ngome ya ulinzi ya Yanga SC, na kufanya matokeo kuwa 3-2.
Yanga SC hawakukubali kuliacha taji la ASFC msimu huu, walisawazisha bao la tatu kupitia kwa Mshambuliaji wake Kinda, Dennis Nkane kwenye dakika ya 113 baada ya purukushani iliyofanywa na Fiston Mayele kwenye lango la Coastal.
Baada ya dakika 120 kuisha, timu hizo zilienda kwenye changamoto ya mikwaju ya Penalti ambapo Yanga SC walipata Penalti zote Nne huku Coastal Union FC wakipata Penalti Moja pekee kwenye mikwaju hiyo.
Coastal Union FC wameshindwa kuwa Mabingwa wa Michuano hiyo ya ASFC, hivyo hawatakuwa sehemu ya Michuano ya Kimataifa msimu ujao, ambapo licha ya Yanga SC kutwaa ubingwa huo, Tanzania itawakilishwa na timu nne ambazo ni Yanga SC, Simba SC watakaowakilisha nchi kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC, Geita Gold FC wakiwakilisha kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments