Na Godwin Myovela, Singida
MAANDALIZI yaliyosheheni shamrashamra za hamasa kuelekea kilele cha Jubilei ya miaka 50 Jimbo Katoliki Singida ifikapo Agosti 21 mwaka huu yamezidi kushika kasi, ambapo moja ya tukio la kuvutia ni namna timu ya mapadri walivyoonesha vipaji vya aina yake kwenye kucheza mpira wa soka kati yao na walei ndani ya uwanja wa Liti mkoani hapa, na hatimaye kufanikiwa kuichapa timu ya walei mabao 5-2.
Kuvuta kamba kati ya timu ya Masista na Wakinamama Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ulikuwa ni mchezo mwingine uliotikisa maandalizi hayo na kuleta ushindani mkali huku shangwe zikitawala uwanja mzima-lakini hata hivyo mwishoni kabisa masista walishindwa kutetea ushindi huo kwa 2-1.
Michezo mingine iliyotawala tamasha hilo kuelekea jubilei ilikuwa ni mchezo wa kuvuta kamba kati ya mapadri na walei, kufukuza kuku na ule wa soka uliodumu kwa dakika 90, ambao kabla ya kuanza ulizinduliwa kwa penati nzuri iliyopigwa na Makamu wa Askofu Pd Francis Limu, ambayo hata hivyo penati hiyo ilifanikiwa kudakwa kwa mbwembwe na Mhasibu wa Jimbo hilo Pd Bernard Ngalya.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa tamasha hilo Pd Limu alisema lengo hasa la michezo hiyo sio mashindano bali ni kuhamasisha kuelekea jubilei na kuonyesha umoja na mapendo kati ya wakristu wa Taifa la Mungu ndani ya Jimbo hilo kwa kuzingatia michezo inaleta furaha, amani na inajenga nguvu.
“Nawaalika wote siku ya Agosti 21 ambayo ndio kilele cha Jubilei, na tunatarajia siku hiyo kupata ugeni mkubwa nchi nzima, wakiwemo viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na wote wenye mapenzi mema kuja kushiriki nasi katika kusherehekea jubilei ya miaka 50 ya Jimbo letu la Singida,” alisema Pd Limu.
Hata hivyo, Mhasibu wa Jimbo hilo Pd Ngalya pamoja na kumshukuru Mungu na kuzidi kuomba baraka kufuatia mwenendo mzuri wa maandalizi kupitia kamati husika unavyoendelea mpaka sasa, alisema kwa hakika miaka 50 ni miaka ya kujivunia.
“Kama Jimbo ndani ya miaka hii limefanya mengi katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utume kupitia huduma za afya, elimu na mambo mbalimbali ya kijamii…tuna kila sababu ya kushangilia jubilei yetu, leo tumefurahi kwenye Misa Takatifu na tunafurahi pia kwenye michezo hapa uwanjani. Naamini basi, Mungu anazidi kutubariki kuelekea Jubilei yetu ambayo inabebwa na kauli isemayo JUBILEI SINGIDA-UMOJA NA MAPENDO,” alisema Pd. Ngalya.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments