TIMU ya Soka ya watoto Mtaani imeingia kambini kwa ajili Maandalizi ya kuelekea Kombe la Dunia la Mtoto wa Mitaani (SCWC) 2022 yatakayofanyika Doha Nchini Qatar.
Mashindano hayo yanayotarajiwa kutimua vumbi kuanzia Oktoba 05 hadi 15 yatakuwa na ushindani mkubwa huku viongozi wa timu hiyo wakifanya kazi kwa bidii ili kupata mafanikio wakati wa shindano.
Ushiriki wa Tanzania katika Mashindano hayo yanatoa jukwaa kwa watoto wa mitaani waliotolewa kutoka mataifa mbalimbali duniani kushiriki katika mashindano ya kandanda ambayo hufanya kama lango la maisha yao ya baadaye.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa timu hiyo Frugence Novatus alisema hadi sasa kila kitu kambini kinaendelea vizuri na kwamba anafanya kazi kwa bidii ili kuwavutia.
“Tumepiga kambi mapema ili wachezaji wapate nafasi ya kutosha ya kuwa pamoja kwa muda mrefu na kuelewana vyema.
"Tuna deni la kufanya vizuri katika mashindano hayo ili bendera ya Tanzania iendelee kung'aa kwenye ramani ya dunia hivyo ili kufanikisha hilo, tunafanya mazoezi mazito," amesema.
Ameongeza, kuwa hadi sasa wana kikosi cha wachezaji 18 kambini ambacho kitapunguzwa na kuwa na wachezaji 10 ambao ni idadi ya wanaotakiwa kufanya safari ya Doha.
Kwa upande wake Mdhamini Mkuu wa Timu ya watoto wa Mtani kutoka kampuni Mansoor Industries Limited (MOIL) Altaf Hiran amesema wameona ni vyema kushirikiana na timu hiyo na kusaidia katika kufikia malengo yao.
“Kama MOIL, huwa tunajitokeza kusaidia katika kazi mbalimbali za jamii na nichukue fursa hii kuwasihi Watanzania daima kuwa mstari wa mbele kuunga mkono masuala mbalimbali yanayotokea katika jamii tunamoishi ili kukuza maisha ya watu.
"Serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu hivyo tunapaswa kuwa tayari kutoa msaada popote pale panapohitajika kufanya hivyo na watoto hawa wana uwezo wa kufikia mambo makubwa iwapo watapata usaidizi unaofaa. Tunataka waishi maisha mazuri pia," Hiran ambaye pia ni rais wa Tanzania Street Children Sports Academy amesema.
Pia, mwanzilishi wa akademi hiyo Mutani Yangwe aliangazia kuwa kando na kuwapa wachezaji jukwaa la kucheza soka, pia wanasaidia kutengeneza maisha yao.
"Baadhi yao hupata fursa za kuendelea na masomo ambayo ni msingi kwa ustawi wao wa baadaye," alisema.
Ikumbukwe kuwa Timu ya taifa ya Tanzania kwa watoto wa mitaani imenyakua Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani, mwaka 2014 katika mashindano yaliyozishirikisha timu za mataifa mbalimbali duniani huko Rio de Janeiro, Brazil.
Timu hiyo imefanikiwa pia kutinga fainali za Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani kwa mara ya mbili mfululizo, na kufanikiwa kutwaa Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani kama linavyojulikana Street Child World Cup.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments