BURIANI KIAMUANGANA MATETA ‘VERCKYS’ | ZamotoHabari

Na Moshy Kiyungi, Tabora.
TASNIA ya muziki wa dansi imepata pigo jingine baada ya mwanamuziki maarufu Kiamuangana Mateta ‘Verkys’ kufariki dunia Oktoba 13, 2022 jijini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiwa na umri wa miaka 78 baada kuungua ugonjwa wa Kiharusi kwa kipindi kirefu.

Wakati wa uhai wake alimiliki bendi ya Orchestra Veve na studio ya kurekodi nyimbo ya Veve Edition katika jiji la Kinshasa nchini Zaire wakati huo, pia alizisaidia bendi za Orchestra Kiam na Orchestra Lipua Lipua ambazo zilikuwa taaban kifedha, alitumia uzoefu wake kibiashara akawa anazichukua nyimbo zao hadi Ulaya kuzirekodi kwa gharama zake.

Wasifu wa mkongwe huyu unaeleza kwamba alizaliwa Mei 19, 1944 katika Kijiji cha Kisatu nje kidogo ya jiji la Leopoldville nchini Kongo Belgium, akapewa jina la George Kiamungana

Wazelambongo Mateta.
Ikumbkwe kwamba nchi hiyo ilitwaliwa na Wakoloni wa Kibelgiji hadi ilipopata Uhuru ikawa Jamhuri ya Kongo Leopoldville chini ya rais Joseph Kasavumbu, baadae alipinduliwa na Joseph Mobutu akaibadili jina la nchi ikaitwa Zaire na mji mkuu wa Leopoldville, ukawa Kinshasa hata jina lake akajiita Mobutu Seseseko Kuku Ng’endu Wazabanga.

Hata hivyo, rais huyo nae alipinduliwa na Laurent Desire Kabila akawa rais wa nchi naye akaibadili jina ikawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kiamungana Mateta wakati akiwa mvulana mwaka 1963 alianza muziki rasmi katika bendi ya Konga Jazz iliyokuwa ikioogozwa na mpiga gitaa Paul Dewayon Ebengo ambae alikuwa mwanamuziki mkubwa nchini humo na ndiye aliyegundua kipaji cha Franco Luambo Luanzo Makiadi.

Baada ya kujiamni kwamba amekomaa katika muziki, mwaka 1965 Verkys aliachana na Ebengo akaenda kujiunga katika bendi ya Tout Puisant Orchestra Kinnie Jazz (T.P. OK Jazz) iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luambo Luanzo Makiadi ambako alikabidhiwa saksafoni ambayo aliimudu kwa kiasi kikubwa.

Akiwa katika bendi hiyo nyimbo zake alizotunga hazikupewa sifa kubwa hadi alipotoa mchango mkubwa kwa ‘kupakua’ vibao vilivyompandisha chati miaka hiyo vya Polo, Bolingo ya Bougie, Ngai Marie na Nzoto Ebeba. Pia alitunga kibao kingine kilichojulikana kwa jina la Oh Madame de la Maison kikiwa na maana ya ‘Mke wa nyumbani’.

Hata hivyo, mkongwe huyu hakudumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo ya T.P. OK Jazz, mwaka 1969 aliamua kuunda bendi yake ya Orchestra Veve iliyowajumuisha wanamuziki wakubwa waliokuwa wamechipukia katika muziki wakati huo akina Matadidi Mabele ‘Mario’, Marcel ‘Djeskain’ Loko na Bonghat ‘Sinatra’ Tshekabu.

Vijana hao miaka michache baadae waliondoka kwenda kuunda bendi yao waliyoiita Trio Madjesi (Sosoliso) ambao ilipata umaarufu mkubwa na ikawa tishio kwa bendi kubwa nchini humo.

Miaka ya 1970 bendi hiyo ya Orchestra Veve ilirekodi vibao vingi kikiwemo alichotunga mwenyewe cha Nakomitunaka kikiwa na maana ya “Najiuliza mwenyewe Mungu tumekosea wapi”, ambacho kilimuweka matatizoni ambapo viongozi wa dini wakituhumu kwaba kinamdhalilisha mungu.

Bendi hiyo ilipata mafanikio makubwa na ilikubalika na watu wengi walipiga muziki maridhawa katika kumbi mbalimbali za jiji hilo na viunga vyake na kwamba ilianza kuweka matawi maeneo mengine ya kibiashara nchini Zaire.

Aidha Verkys alimiliki bendi ya Orchestra Veve na studio kubwa ya kurekodi miziki ya Veve Edition katika jiji la Kinshasa pia alizisaidia bendi za Orchestra Kiam na Orchestra Lipua Lipua ambazo zilikuwa taaban kifedha, akatumia uzoefu wake kibiashara akawa anachukua nyimbo zao hadi Ulaya kuzirekodi kwa gharama zake.

Mkongwe huyu alikuwa alijulikana kwa jina hata bila ya yeye kuwepo jukwaani na alipenda kutumia muda mwingi kujenga mtandao katika klabu akirekodi nyimbo katika studio yake ya kisasa ya kurekodi muziki aliyoifungua mwaka 1972 katika Jiji la Kinshasa.

Miaka ya 1980 Verckys alikuwa tishio kwa wanamuziki wakubwa nchini humo, akiwemo Franco Luanzo Makiadi na Tabu Ley Rochereau kwa kuweza kumudu muziki wa watu wa Kongo pamoja na kufanya biashara kadhaa za Kimataifa.

Baadhi ya watu walidai kwamba Kiamuangana alikuwa na ‘mapafu ya mbwa’ kufuatia uwezo wake mkubwa wa kupuliza saksafoni ambaye takriban nyimbo zote za bendi yake alipuliza ala hiyo.

Verkys pia alianzisha bendi zingine nyingi zikiwemo za Les Grands Maquisards na Orchestra Bella Bella zikiwa na nembo ya Veve Edition na mwaka 1978 aliandaa makao makuu ya burudani yakajulikana kama Veve Centre na mwaka huohuo alichaguliwa kuwa rais wa Umoja wa Wanamuziki Zaire (UMUZA) hadi anaaga dunia Verkys bado alikuwa mwanachama wa umoja huo.

Verkys akiwa rais wa UMUZA alitumia nafasi yake hiyo kuja nchini kuchunguza baadhi ya nyimbo za bendi za wanamuziki wa nchi yake ya Zaire zilizodurufiwa na baadhi ya bendi za Tanzania miaka hiyo.

Mfano ni wimbo wa ‘Mokolo Nakokufa’, Wanamuziki wa Tanzania wakauita Lua nafasi, wimbo wa Est –ce que Oyimbi akapewa jina Nacheka Kilwa leo na Maneno hayafai, wimbo wa Course au Povouir ukaitwa Roza Waua na nyingine kadhaa.

Aidha miaka ya 1980 Kiamuangana Mateta ‘Verkys’ alisaidia uanzishwaji wa bendi za vijana waliokuwa wakichipukia wakati huo za Langa Langa Stars, Victoria Eleison waliokuwa wakipiga muziki wao kwa mtindo wa ‘Kidekule’ na Anti-Choc wakipiga kwa mtindo wa ‘Nzawisa’.

Akiwa na bendi yake ya Orchesta Veve aliachia vibao vilivyowakamata wapenzi na mashabiki wa muziki wakati huo ambavyo hadi sasa hurindima kweye baadhi ya vituo vya redio nchini vya Baluti, Lukani, Mama na Fuki, Ndona, Yanini, Zonga Andowe, Mikolo mileki mingi, Vivita, Basala Hot, Asamba, Mabuse, Yanini, Ndona, Nakomitunaka na Djumani.

Zingine ni Taty, Emmission Sekere Recoite, Maza, Mangala, Muana Mburu, Okendeke Malamu, Fifi na Nakoma Juste.

Aidha alirekodi na kutoa albamu akiwa na baadhi ya bendi nyota katika muziki zikiwemo za Empire Bakuba, Victoria Eleison na Langa Langa Stars.

Kufuatia ongezeko la shughuli na majukumu yaliyombana, alijikuta anakosa muda wa kushiriki kikamilifu katika kupiga muziki hadi kufikia bendi hiyo kuporomoka hadi kutoweka kwenye sura muziki.

Mhenga George Kiamungana Wazelambongo Mateta 'Verckys' nyimbo zake zitadumu kwa kipindi kirefu kufuatana na ujuzi wa wanamuziki waliumganisha mawazo yao na kuifanya Orchestra Veve kuwa kubwa kimuziki.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba 0767331200, 0713331200, 0736331200 na 0784331200.
KIAMUNGANA MATETA 'VERCKYS' AKIPULIZA SAKSAFONI JUKWAANI.
BURIANI KIAMUANGANA MATETA ‘VERCKYS’ AKIFANYA VITU VYAKE MITAANI.
BURIANI KIAMUANGANA MATETA ‘VERCKYS’.AKITUZWA NA KIMWANAJUKWAANI.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini