KIKOSI cha wachezaji 24, viongozi pamoja na benchi la ufundi leo wameanza safari ya kuelekea Jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wa ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa siku ya Jumanne Novemba moja katika Uwanja wa CCM Kirumba Jijini hapo.
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana ikiwa Jijini Mwanza mbali na mchezo huo dhidi ya Kagera Sugar ,pia itacheza mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Geita Gold ambao utapigwa katika uwanja wa Nyankumbu Novemba 11 mkoani Geita.
KMC FC kabla ya kuanza safari ya kuelekea Jijini Mwanza, ilikuwa ikiendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo ikiwa ni tangu ilipotoka kupoteza mchezo wake wa Oktoba 26 dhidi ya Yanga katika uwanja wa Benjamini Mkapa na kwamba maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia kubwa.
Wachezaji wote wa KMC FC wameondoka wakiwa na hari, morali nzuri na kwamba hakuna mwenye changamoto huku kila mmoja akiwa amejiandaa kwa mchezo huo ili kuwapa furaha mashabiki na wapenzi wa Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni licha ya ushindani uliopo kwenye michezo hiyo miwili Kanda ya Ziwa.
Katika msafara huo, KMC imebakiza wachezaji watatu ambao wataendelea na programu za mazoezi kadiri ambavyo Kocha Hitimana amewaachia ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa wakati wakisubiria kufanya maandalizi mengine pale Timu itakaporejea Novemba 12.
“Tunakwenda kanda ya Ziwa kucheza mechi mbili ambazo kimsingi tunafahamu kabisa zitakuwa na ushindani mkubwa ukizingatia kila Timu hivi sasa inahitaji kupata matokezo mazuri lakini sisi tumejiandaa vizuri kukabiliana na ushindani huo.
Ukiangalia mwenendo wa Ligi hadi sasa ushindani kwa kila Timu unaongezeka siku hadi siku, kila mmoja anataka kufanya vizuri kwenye mchezo wake haijalishi yupo nyumbani ama ugenini, kwahiyo hata KMC tunahitaji kufanya vizuri lakini pia tunakwenda kanda ya ziwa tukiwa na tahadhari zote sambamba na kuwaheshimu wapinzani wetu.
KMC FC ikiwa jijini Dar es salaam, imecheza jumla ya michezo mitano na kufanikiwa kushinda jumla ya michezo mitatu ambayo ilikuwa nyumbani na kusare michezo miwili ambayo kati ya hiyo mmoja ikiwa nyumbani na mwingine ikiwa ugenini huku ikipoteza mchezo mwingine mmoja ikiwa ugenini pia.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments