Michezo ya SHIMIWI yaendelea kunoga Jijini Tanga | ZamotoHabari

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MICHEZO ya Shirikisho la Michezo ya Wiraza na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI), imeendelea kunoga kwa timu kuonesha burudani nzuri kwa wananchi wa Tanga kwa michezo mbalimbali.

Kwa upande wa soka, timu za soka za Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Maji, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB) pamoja na RAS Simiyu zimeng’ara kwa kufanya vizuri kwa kuwachabanga wapinzani wao na kujizolea pointi tatu kila mmoja.

Timu ya Wizara ya Maji ilimeichabanga RAS Mara kwa jumla ya magoli 4-1, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamefunga RAS Lindi magoli 2-0, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB) imewafunga Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa jumla ya magoli 2-0 huku RAS Simiyu wakitakata kwa kuifunga timu ya Wakala wa Taifa wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa goli 1-0.

Akizungumzia ushindi wa timu yake Mwenyekiti wa klabu ya PCCB Bw. Denis Manumbu ambaye pia ni Mwalimu wa timu hiyo amesema wamefanikiwa kuwafunga wapinzani wao baada ya kuwasoma na kutumia winga zaidi hatua iliyowafanya wapoteneane na wao kufunga magoli 2-0 na sasa wanajinpanga kwa mechi zinazofuata.

Naye mwalimu wa timu ya Wizara ya Maji ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga UWASA Mhandisi Geofrey Hilly amesema wameonesha makeke kwa timu ya RAS Mara kwa kuwapiga kwa goli 4-1.

“Tunafuraha kubwa kwa kweli na tumepata hamasa katika kundi letu, tayari tunaongoza tunahamasa ya kutosha tunategemea sasa sisi ni lazima tuendelee mbele, tunaishukuru Wizara kwa kutuwezesha kufanikisha timu kushiriki mashindano haya kwa hamasa kubwa” amesema Mhandisi Geofrey.

Katika mchezo wa kamba uliowavutia watazamaji wengi, kwa upande wa wanaume timu zilizoshinda mivuto 2-0 ni Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari waliwavuta Wizara ya Sheria na Katiba; nao Wizara ya Mambo ya Ndani waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi); huku Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waliwavuta RAS Shinyanga; na Idara ya Mahakama waliwavuta RAS Singida; huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliwavuta RAS Simiyu; huku Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini nchini (GST) waliwavuta RAS Lindi.

Timu nyingine za wanaume zilizoshinda kwa mivuto 2-0 ni nayo Ofisi ya Ukaguzi wa Taifa waliwavuta Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; nao Wizara ya Kilimo wamewavuta Wizara ya Maji; Hazina waliwavuta Bohari ya Dawa (MSD); nazo timu zilizoshinda kwa mvuto mmoja baada ya mvuto wa awali kutoka sare ni RAS Dodoma waliwashinda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala; wakati zilizopata ushindi wa chee baada ya wapinzani wao kutoonekana uwanjani ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo walipata ushindi dhidi ya Wakili Mkuu wa Serikali nayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipata ushindi dhidi ya RAS Manyara.

Kwa upande wa wanawake timu zilizoshinda kwa mivuto 2-0 ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waliwashinda Wizara ya Mambo za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; nayo Wizara ya Katiba na Sheria waliwashinda Bohari Kuu uya Dawa; wakati Ofisi ya Waziri Mkuu waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi); nao Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora waliwavuta Wizara ya Kilimo; wakati Wizara ya Mifugo waliwavuta Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; huku Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) waliwashinda RAS Mbeya na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) waliwashinda RAS Dodoma.

Timu zilizoshinda kwa mvuto mmoja ni Hazina waliwashinda Wizara ya Elimu; Wizara ya Mambo Ndani waliwashinda RAS Simiyu; nayo RAS Tanga waliwashinda Ofisi ya Waziri Mkuu Sera; huku timu zilizopata ushindi wa chee baada ya wapinzani wao kuingia mitini ni RAS Singida dhidi ya RAS Kilimanjaro; RAS Iringa dhidi ya RAS Dar es Salaam; Wizara ya Madini dhidi ya RAS Ruvuma.

Katika mchezo wa netiboli uliofanyika kwenye uwanja wa Bandari timu ya Ulinzi waliwachabanga bila huruma RAS Njombe kwa kuwafunga magoli 52-1. Hadi mapumziko washindi waliongoza kwa magoli 31-0; nao Wizara ya Elimu waliwashinda Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa magoli 25-8. Elimu walikwenda mapumziko kwa magoli 11-6; huku Wizara ya Afya waliwaadabisha Wizara ya Nishati kwa magoli 44-6.

Mechi zilizofanyika kwenye uwanja wa Polisi Chumbageni timu ya Wizara ya Kilimo waliwafunga RAS Mtwara kwa magoli 35-3; nao Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) waliwachapa Ofisi ya Bunge kwa magoli 33-25; huku Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari walitoka sare na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwa magoli 14-14; nayo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) waliwashinda Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi kwa magoli 29-9.



Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini