NYANDA KUTOKA BRAZIL ATAJWA KUWASHA MOTO SIMBA SC | ZamotoHabari


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Golikipa raia wa Brazil, Caíque Luiz Santos da Purificação ametajwa kutua Simba SC ya Tanzania msimu ujao wa mashindano, baada ya timu hiyo kutafuta Golikipa ambaye atakuwa mbadala wa Kipa namba moja, Aishi Manula ambaye ni majeruhi.

Caíque Luiz mwenye Futi 6 alizaliwa mwaka 1997 huko Salvador nchini Brazil, aliwahi kucheza timu ya taifa ya vijana ya nchi hiyo, kabla ya tetesi kuhusishwa kujiunga na Simba SC, Caíque Luiz alikuwa anacheza Ypiranga FC ya nyumbani kwao Brazil.

Tetesi za Waandishi wa Habari za michezo barani Afrika zimeripoti kuwa Golikipa huyo yupo kwenye mawindo ya Mnyama (Simba SC) ili msimu ujao awasaidie kulinda lango lao kwenye mashindano ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na mashindano mengine ya ndani.

Pia Simba SC itakuwa inacheza mashindano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) na mashindano ya CAF Super League ambayo yametajwa kuanza kutimua vumbi mwezi Oktoba mwaka huu, yakishirikisha miamba ya soka barani Afrika.

Simba SC ipo mawindoni kutafuta mrithi wa Manula ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi minne kuuguza majeraha yake ya Nyama za Paja na tayari amepatiwa matibabu nchini Afrika Kusini. Simba SC ipo na Golikipa namba tatu pekee, Ally Salim na tayari imeagana na Golikipa wake namba mbili, Beno David Kakolanya.

Caíque Luiz anayetajwa kutua Simba SC amewahi pia kucheza Klabu za Esporte Clube Vitória (Brazil), amecheza kwa mkopo, timu za Centro Sportivo Alagoano (Brazil), Ermis Aradippou (Cyprus) na Rochester New York FC (Marekani).



 

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini