KUAMBIANA CUP YAANZA KULINDIMA | ZamotoHabari




Na. Damian Kunambi, Njombe.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana amezindua ligi ya kuambiana CUP katika tarafa ya Masasi ambapo katika uzinduzi huo ameziasa halmashauri zote nchini kuanzisha ligi mbalimbali kwa vijana ili vipaji vyao viweze kuonekana na waweze kunufaika na fursa zilizopo ndani ya wizara hiyo.

Akizindua ligi hiyo katika viwanja vya Ngelenge vilivyopo katika kata ya Ruhuhu wilayani Ludewa Mkoani Njombe Waziri Chana amempongeza mwandaaji wa ligi hiyo Imani Haule (Kuambiana) kwa kukusanya vijana na kuibua vipaji na kumtaka kuwasilisha wizarani majina ya wachezaji watakao onekana kuwa na vipaji zaidi.

"Wizarani kuna fursa nyingi zinazohitaji vijana wenye vipaji, sasa niwaombe Kuambiana CUP pamoja na Kamonga CUP mniletee majina ya vijana watakao onekana kuwa na vipaji pamoja na taarifa zao juu ya maeneo wanayotoka ili waweze kupata fursa zilizopo na kuinua vipaji vyao zaidi". Amesema Balozi Dkt. Pindi Chana.

Aidha kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva pamoja aliwataka vijana wanaoshiriki michuano hiyo ya Kuambiana kutumia vyema vursa hiyo kwa kuonyesha vipaji vyao sambamba na nidhamu katika mchezo.

Joseph Kamonga ni mbunge wa jimbo la Ludewa amesema kwa miaka mitatu mfululizo amekuwa akishirikiana vyema na Kuambiana katika mashindano hayo ambapo ameahidi kuendeleza ushirikiano huo walionao ili kuwainua vijana.

Hata hivyo kwa upande wake Kuambiana amesema mashindano hayo yamekuwa yakibadilika kila mwaka ambapo hutanua wigo zaidi ambapo awali walikuwa wakiyafanya kwa Tarafa ya Masasi wilayani Ludewa na Nyasa mkoani Ruvuma lakini kwa mwaka huu wilayani Ludewa wameongeza Tarafa ya Mawengi.


"Mashindano haya yamelenga kuibua vipaji vya vijana na tumekuwa tukifanya maboresho kila mwaka, ninashukuru kuona tangu nianzishe ligi hii kumekuwa na mafanikio kwa baadhi ya wachezaji kwani vipaji vyao vimeweza kuonekana na kusajiliwa katika Club mbalimbali hapa nchini". Amesema Kuambiana.

Mashindano haya kwa sasa yamefikisha msimu wa nne tangu kuanzishwa kwake ambapo kwa msimu huu katika ufunguzi timu ya Ilela kutoka wilaya ya Ludewa mkoani Njombe ilikipiga na timu ya Nkaya kutoka wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na kupelekea timu ya Nkaya kuibuka kidedea kwa kuifunga Ilela kwa magoli 3 kwa moja na kujinyakulia Kombe, kitita cha sh. Laki tatu na nusu, medali, jezi pamoja na mpira huku Ilela ikipata kitita cha sh. Laki mbili na nusu,medali,jezi na mpira.




















Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini