KWA TETESI NA VYUMA HIVI …! MSIMU WA LIGI UANZE TU …!!! | ZamotoHabari






Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KUMEKUWA na tetesi nyingi za usajili katika soka nchini Tanzania kuelekea msimu ujao wa mashindano (2023-2024), baadhi ya wachezaji wamekuwa wakitajwa sana kwenye tetesi hizo, lakini tetesi nyingine ni za kweli na nyingine ni uongo.

Dirisha la usajili bado lingali lipo wazi tangu kufunguliwa Julai 01 mwaka huu linatarajiwa kufungwa rasmi Agosti 31, mwaka huu. Kumekuwa na mikikimiki mingi sana kwenye usajili huo haswaa kwa timu kongwe nchini yaani, Yanga na Simba.

Si ajabu! kwa timu hizo kuhusishwa kwenye tetesi hizo, tena kwa wachezaji wenye uwezo na mahiri katika kulisakata kabumbu, kwa wale wachezaji waliocheza kwenye Klabu hizo na wale wasiocheza yaani walikuwa wanatumikia timu nyingine nje na ndani ya Tanzania, tetesi hizo zinawahusu sana.

Hivi karibuni kumekuwa na soga zinazomuhusu Nyota mahiri wa Simba SC, Mzambia Clatous Chota Chama kusajiliwa na Wananchi, Yanga SC, soga hizo ni tetesi tu! ingawa inadaiwa Chama bado ni mali ya Mnyama, Simba SC kwa mujibu wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally.

Huku na kule, Mzambia huyo hadi hivi tunavyozungumza bado hajajiunga na wenzake waliopo kambini Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2023-2024. Kikosi cha Simba SC kipo kwenye ardhi ya Uturuki chini ya Kocha Mkuu, Robertinho (Mzee wa Samba Roketo) kikijinoa kwa ajili ya msimu mpya.

Watoto wa mjini wanasema haijaisha hadi iishe! dirisha la usajili bado lipo wazi, wahusika wenyewe watatoka mbele ya umma na kuja kuthibitisha kila kitu ijapokuwa hii ni kazi yetu sisi vyombo vya habari kutoa taarifa kwa umma kuhusu sajili hizo za wachezaji mbalimbali.

Mnyama, tayari ameshusha chuma kingine kutoka DR Congo, Fabrice Ngoma ambaye alikuwa kwenye Klabu ya Al Hilal ya Sudan. Hii ni baada ya kukamilisha usajili wa Nyota Aubin Kramo Kouamé, Che Malone Fondoh, Willy Essomba Onana na kumrudisha nyumbani, David Kameta (Duchu).

Simba SC walihusishwa kuwapora Yanga SC, Mchezaji Fabrice Ngoma kwenye uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ikiwa ni baada ya kutua nchini, hizo ni tetesi tu! hakuna aliyethibitisha kwa asilimia 100% kuwa mchezaji huyo aliporwa ‘Airport’.

Huku wakiwaongezea mikataba hadi mwaka 2025 Walinzi wake wa pembeni, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein (Zimbwe Jr) wote kwa pamoja watamaliza mikataba yao mwaka huo wa 2025.

Pia, wamesajili Meneja wa timu na Sayansi ya michezo, Mikael Igendia, Kocha wa Magolikipa, Daniel Cadena (ametoka Azam FC), Mtaalamu wa mazoezi ya viungo (Fitness Coach), Corneille Hategekimana.

Wananchi, Yanga SC wanaendelea na usajili na tayari wamenyakua mtu mmoja mmoja aliyeachwa na Simba SC, Jonas Mkude (Nungu nungu), Yanga SC wamemsajili Mkude na Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate FC huku wakitangaza usajili wa Mlinzi wa kigeni kutoka Uganda, Gift Fred.

Wananchi hawajaishia hapo, wametangaza chuma kingine kutoka DR Congo, Maxi Mpia Nzengeli. Tayari wametangaza Kocha Msaidizi, Mousa Ndoa kutoka nchini Senegal ambaye atasaidiana na Kocha Mkuu, Miguel Angel Gamondi kutoka nchini Argentina.

Siku ya Mwananchi, Julai 22, 2023 watakuwa na kibarua kizito dhidi ya miamba ya soka kutoka Afrika Kusini, Kaizer Chief (Amakhosi) wakatua nchini Tanzania kwa ajili ya kusherehesha sherehe hizo katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini