SPORTPESA WAMETUNYANYUA - SINGIDA FOUNTAIN GATE FC | ZamotoHabari

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Uongozi wa Singida Fountain Gate FC umesema kuwa udhamini wa Kampuni ya michezo ya kubashiri (Sportpesa) umekuwa chachu kubwa ya wao kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali hususani Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu ulioisha wa 2022-2023.

Sportpesa imetoa ‘bonasi’ la Shilingi Milioni 50/- (Tsh. 50,000,000) kwa timu hiyo baada ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara wakimaliza kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam baada ya kupokea kitita hicho, Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, John Kadutu wameshukuru kupata ‘bonasi’ hilo, huku akibaisha kuwa msimu ujao watawasha moto na kuhakikisha wanamaliza Ligi wakiwa kwenye nafasi nzuri za juu na kufanya vizuri mashindano mengine wanayoshiriki.

“Sportpesa tunawashukuru sana kutupa ‘bonasi’ hili, hii ni kama motisha kwetu kuhakikisha tunafanya vizuri msimu ujao wa 2023-2024, kutokana na udhamini wa Sportpesa, tumekuwa nao bega kwa bega na ndio maana kwa muda mfupi tulioshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, tumefanya vizuri na kuwa nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu,” amesema Kadutu.


“Kwa hakika, mkiona mafanikio katika Klabu yetu ya Singida Fountain Gate, basi tambueni kuwa nyuma yetu ipo Kampuni ya michezo ya kubashiri ya Sportpesa, tumenufaika sana na udhamini huu,” ameeleza Kadutu.


Vile vile, Kadutu amesema kuwa kwa sasa baada ya Sportpesa kuingia kwenye udhamini wa baadhi ya vilabu, kumekuwa na faida kubwa kwenye vilabu hivyo kutokana na kunufaika na udhamini huo, huku akibainisha kuwa vilabu hivyo sasa vinatembea kifua mbele kutokana na uwepo wa fedha.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas amesema wametoa ‘bonasi’ hilo kwa Singida Fountain Gate FC ili iwe chachu kwao kufanya vizuri zaidi katika mashindano wanayoshiriki msimu ujao.


“Tumetoa Shilingi Milioni 50/- kwa Singida Fountain Gate FC kama ‘bonasi’, wamefanya vizuri kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu ulioisha (2022-23) na sio kazi rahisi kupanda Ligi Kuu msimu mmoja tu na kuwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo,” amesema Tarimba.


Hata hivyo, Tarimba amewataka Singida Fountain Gate FC kutobweteka na mafanikio hayo, huku akitoa wito kwao kufanya vizuri zaidi kwenye msimu ujao. Pia, Tarimba amesema wanajivunia kuwa na mafanikio makubwa kwenye udhamini wa baadhi ya vilabu vya soka nchini.


“Sportpesa tunadhamini timu tatu kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, tunawadhamini Yanga SC ambao walikuwa Mabingwa wa msimu uliopita, tunawadhamini Singida Fountain Gate FC ambao walimaliza nafasi ya nne na Namungo FC ambao walimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo,” ameeleza Tarimba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas (wa kushoto) akikabidhi kitita cha Shilingi Milioni 50/- kwa Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Singida Fountain Gate FC, John Kadutu (wa kulia).


Sportpesa imekabidhi fedha hizo kama ‘bonasi’ kwa timu hiyo baada ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu ulioisha wa 2022-2023, ikimaliza Ligi hiyo katika nafasi ya nne.





Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini