WAZIRI MKUU AIPONGEZA KAMPUNI YA INSIGNIA KUIDHAMINI NAMUNGO FC | ZamotoHabari

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa ameishukuru kampuni ya Insignia Limited kupitia rangi zake za Coral Paints kwa kuidhamini timu ya Namungo FC iliyopo jimboni mwake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Akizungumza kwenye hafla ya kusaini makubaliano ya udhamini na uzinduzi wa jezi mpya kati ya kampuni ya Insignia Limited na uongozi wa timu ya Namungo katika uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi siku ya Jumanne usiku, Majaliwa amesema timu hiyo imejiandaa vizuri ili kuleta ushindani msimu huu.

”Tumejiandaa vizuri na vijana ( wachezaji) sasa hivi wapo kambini mkoani Arusha kwa ajlli ya kambi ya maandalizi, huku usajili ukifanyika kimya kimya,”


" Tunawashukuru sana Coral Paints kwa kutupa nguvu kubwa Namungo kuelekea msimu ujao ili tufanye vizuri katika ligi na michuano ya kimataifa endapo tutamaliza msimu huu katika nafasi za juu kabisa," amesema


Katika msimu uliomalizika, Namungo ilimaliza katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 40 na kukosa tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu Afrika ambayo Tanzania itawakilishwa na Simba, Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam na Singida Fontain Gate zitacheza Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema timu hiyo imeweka mipango madhubuti ikiwemo kuimarisha uhai wa matawi ya wanachama na kutafuta vyanzo mbalimbali vya kujiingizia mapato ikiwemo kupitia mauzo ya jezi na sapoti kubwa kutoka kwa wana Ruangwa wenyewe na wadau wengine mbalimbali wakiwemo Coral Paints ili waweze kufanya vizuri zaidi msimu huu.

Waziri Mkuu amesema licha ya nafasi mbili za juu kuwa ngumu kwa sababu mara nyingi zinashikiliwa na Simba na Yanga, lakini amesema ana Imani Namungo, au ’ Wauaji wa Kusini’ kama inavyojulikana ipo siku iitatwaa ubingwa huo.


”Zile nafasi mbili za juu zinaweza kuwa mgogoro kwetu, japokuwa tutapambana na ipo siku tutafanikiwa kutwaa ubingwa na ndio malengo yetu,”


” Lakini nafasi hii ya tatu na nne huku hatuna wasiwasi nayo, hii tunaiweza na tutapambana kwelikweli ili tucheze michuano ya kimataifa,” alisema Waziri Mkuu.


” Nguvu kubwa tunayoipata kutoka kwa wadhamini wetu na mashabiki inazidi kutupa matumaini na ari ya kupambana,”.


”Tunawashukuru sana, mara ya kwanza mmetusaidia kukarabati uwanja na sasa mmekuja na udhamini ili kutupa nguvu katika safari yetu ya mafanikio,”amesema Majaliwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Insignia Isaac Kiwango ambaye hata hivyo hakuweka wazi thamani ya udhamini huo, alisema udhamini wa kampuni hiyo ni wa miaka mitatu na umejikita katika maeneo mbalimbali na utakuwa wenye maboresho.

Alisema kampuni yake imedhamini vifaa vya timu hiyo ikiwemo jezi aina tano ambazo timu hiyo imezizindua ikiwa ni kwa ajili ya mechi za nyumbani, ugenini, kirafiki. kombe la Shirikisho na nyingine ya kuitangaza Namungo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Namungo, Twaha Mpembenwe ambaye pia ni Mbunge wa Kibiti naye alisema wanataka kuona namungo inasonga mbele katika Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na hata itakaposhiriki michuano ya kimataifa.

Aliwataka mashabiki, wanachama na wapenzi wa Namungo kuwa kitu kimoja na kwamba mshikamano wao ndio mafanikio ya timu hiyo.

Tayari Bodi ya Ligi imetangaza Agosti 15, kuwa ndio tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu wa 2023/24 huku Yanga ikitetea ubingwa wake iliyoutwaa kwa mara ya pili mfululizo. Mlezi wa timu ya Namungo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya jezi ya timu hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa bodi wa timu hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kibiti Twaha Mpembenwe baada ya kuzinduliwa kwa jezi hizo na kutangaza udhamini wa Coral Paints katika uwanja Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akimkabidhi jezi ya Namungo mdhamini wa timu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Insignia Limited Isaac Kiwango wanaodhamini timu hiyo kupitia rangi za Coral Paints wakati wa kutangaza udhamini huo Ruangwa mkoani Lindi
Warembo wakionyesha jezi mpya za Namungo FC zitakazotumika katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakati wa uzinduzi uliofanyika katika uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini