MNYAMA ASHUSHA NYANDA KUTOKA MOROCCO | ZamotoHabari

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Simba SC imemsajili golikipa Ayoub Lakred raia wa Morocco kwa mkataba wa miaka miwili, Ayoub amewahi kucheza kwenye timu ya AS FAR Rabat ya nchini humo.


Lakred ni golikipa mwenye umri wa miaka 28, amewahi pia kucheza timu ya RS Berkane ya nyumbani kwao Morocco. Akiwa AS FAR Rabat ameiongoza timu hiyo kushinda ubingwa wa Ligi Kuu nchini Morocco msimu uliopita na kufika hatua ya Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.


“Lakred ana uzoefu kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa ambayo tunaamini atakuwa msaada mkubwa,” wamesema Simba SC


Golikipa huyo anakuja kuziba pengo lililoachwa wazi na golikipa raia wa Brazil, Jefferson Luis ambaye alisajiliwa na kuachwa kikosini hapo (Simba SC) kwa sababu iliyotajwa kuwa majeruhi.


Ayoub ataungana na Makipa waliopo, Ally Salim, Hussein Abel na Ahmed Feruz wakati Golikipa namba moja Aishi Manula akiendelea kuuguza majeraha yake.


Hata hivyo, Rais wa Heshima wa Klabu hiyo, Mohammed Dewji alishauri timu hiyo kuongeza golikipa mwengine wakati Aishi Manula akiendelea kupatiwa matibabu.


“Ali ni mzuri na Aishi Manula ni namba moja nchini Tanzania, hata hivyo tunahitaji kushindana kwenye Ligi ya Mabingwa barani Afrika, tunahitaji kuwa na golikipa mwengine,” amesema Mo Dewji.





Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini