NAMUNGO FC YAMWAGIWA MAHELA, KAZI KWAO | ZamotoHabari

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
NAMUNGO FC ya Lindi, Tanzania imepata fedha za udhamini wa Shilingi Bilioni Moja na Milioni Hamsini na Tano (Tsh. 1,055,000,000) kutoka Sportpesa ili kuwawezesha kufanya vizuri zaidi katika msimu wa mashindano wa 2023-2024.

Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba mpya na timu hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas amesema wameboresha mkataba na timu hiyo kuweka kiasi hicho cha fedha ili kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu na mashindano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).

“Sisi tutatoa zawadi za bonasi kwao endapo watafanikiwa zaidi katika mashindano ya Ligi Kuu, ASFC na mashindano ya CAF, kwenye mkataba huu pia endapo watafanya hivyo watapata kiasi kilichowekwa mezani. Kwa ufupi udhamini huu unaenda kuboresha ufanisi wa timu ya Namungo FC,” amesema Tarimba.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Namungo FC, Omar Kaya wameshukuru kupata udhamini huo, amesema udhamini huo ni chachu ya kufanya vizuri kwenye msimu ujao wa mashindano wa 2023-2024.

“Tunawashukuru Sportpesa kutupa udhamini huu, tutahakikisha tunafanya vizuri kwenye msimu ujao wa mashindano lakini pia niwashukuru kuendelea kupigania mafanikio ya soka letu la Tanzania kwa kutoa udhamini kama huu,” amesema Kaya.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kusaini mkataba baina yao na Namungo FC. Wa kwanza kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omar Kaya.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini