Mwandishi Wetu
KUTOKANA na kesi ya Mwanamuziki wa kizazi kipya Lameck Ditto dhidi ya kampuni ya MultiChoice Tanzania Limited, Meneja wake Rodney Rugambo ameieleza Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam namna ambavyo mwanamuziki huyo aliathirika baada ya wimbo wake wa "Nchi Yangu" kutumiwa na kampuni hiyo kwenye matangazo yao ya biashara kipindi cha Kampeni ya Afcon 2019.
Akitoa ushahidi wake, mbele ya jaji mfawidhi, Salma Maghimbi jana, Rodney ambaye ni shahidi wa nne kati ya watano katika kesi hiyo ya madai, alisema amekuwa meneja wa Ditto tangu mwaka 2016.
Alisema, mwaka 2017, Ditto aliandika wimbo huo, wakilenga kuutumia kama nembo (brand) kwenye kampeni ya Kibanda umiza.
"Wimbo ulipotengenezwa, tulikuwa na mpango wa kuitumia kwenye kampeni ya Kibanda umiza," alisema.
Katika ushahidi wake, alidai kwenye kampeni hiyo, katika kipindi cha miaka mitano, Ditto angelipwa Sh 1.8bilioni.
Alisema, kabla ya kuanza kwa kampeni hiyo, waratibu wa Tamasha la urithi, waliuomba kuutumia kwenye tamasha hilo.
"Kwenye tamasha la urithi wimbo huo haukutumika kwa ajili ya kibiashara, tukiwa tunaendelea na mchakato wa kuutumia kwenye kampeni ya Kibanda umiza, tulishangaa kuona DSTV (Kampuni ya MultiChoice Tanzania Limited) wameutumia kwenye matangazo yao ya kibiashara," alisema meneja huyo.
Alisema, jambo lile lilimuathiri Ditto ambaye hakuweza kuendelea kwenye kampeni ya Kibanda Umiza.
"Wimbo wa Nchi yangu haukutumiwa tena kwenye kampeni ile na yeye (Ditto) kushindwa kuendelea na mkataba ule, kwani tayari wimbo ulishatumika kibiashara na kampuni nyingine hivyo thamani yake kushuka," alisema Rodney.
Baada ya kutoa ushahidi wake, mawakili wa Multi Choice Thomas Mathias na Lyimo walimuuliza maswali kadhaa shahidi huyo, ikiwamo endapo anafahamu kuhusu mashindano ya Afcon na shahidi huyo kueleza hajui chochote kuhusu mpira wa miguu.
Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bernard Bwakeya alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mwaka 2020 akiomba iamuru kampuni Multi Choice Tanzania imlipe fidia ya Sh 6bilioni kwa kutumia wimbo wa Nchi Yangu aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake.
Pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe Milioni 200 kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.
Kesi hiyo itaendelea tena Jumatatu, Machi 25 kwa shshidi watano kutoa ushahidi wake Mahakamani hapo, upande wa mshtaka ukiongozwa na mawakili Ally Hamza na Elezabeth John.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments