USHIROMBO WARRIORS WATWAA UBINGWA KNK CUP BUKOMBE 2026 | ZamotoHabari

Timu ya Ushirombo Warriors FC imetwaa ubingwa wa Wilaya ya Bukombe katika mashindano ya KNK CUP 2026, baada ya kuichapa Katome FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa tarehe 7 Septemba 2026 katika Uwanja wa Bukombe Stadium uliopo Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Katente, Tarafa ya Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Ushirombo Warriors walionyesha kiwango kizuri na kutumia vyema nafasi walizopata. Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 43 na mshambuliaji wao Hames Kigwangala kabla ya mapumziko.

Kama mabingwa, Ushirombo Warriors FC walikabidhiwa kombe, seti tatu za jezi, mipira mitatu pamoja na kitita cha shilingi milioni 5. Katome FC ambao walimaliza nafasi ya pili walikabidhiwa seti mbili za jezi, mipira miwili pamoja na shilingi milioni 3. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Msasa FC ambao walikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja pamoja na shilingi milioni 1.

Zawadi hizo zilikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskasi Muragili, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita. Mashindano hayo yanafadhiliwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.

Mratibu wa Kamati ya Mashindano ya KNK CUP 2026 Wilaya ya Bukombe, Bosco Mwidad, alisema mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaibua vijana wenye vipaji vya soka. Alisema tangu mashindano hayo yalipoanza mwezi Julai mwaka huu, jumla ya timu 248 zilishiriki, huku zawadi zikitolewa kuanzia ngazi ya kata hadi tarafa.

Nahodha wa Ushirombo Warriors FC, Damas Buyenze, alieleza furaha yake baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Wilaya kwa mara ya kwanza. Alisema “Nina furaha sana pamoja na wachezaji wenzangu kwa kutwaa ubingwa wa Wilaya, kwani si jambo dogo. Tulijipa moyo, tukajituma na kumsikiliza mwalimu wa timu, na leo tumetwaa ubingwa. Pia namshukuru Mungu kwa kunisaidia kuwa golikipa bora”.

Wananchi wa Bukombe pamoja na wapenda michezo kwa ujumla wamemshukuru Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kuendelea kugharamia mashindano hayo ambayo yamekuwa chachu kubwa ya kukuza na kuibua vipaji vya watoto na vijana katika Wilaya hiyo.












Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini