TAMASHA la Tigo Fiesta 2017 lenye kaulimbiu ya ‘Tumekusoma’, linatarajiwa kuhitimishwa jijini Dar es Salaam Jumamosi hii kwenye viwanja vya Leaders Club, huku wasanii mbalimbali wakali hapa nchini wakisubiriwa kufanya shoo ‘bab kubwa’.
Miongoni mwa wasanii wanaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa muziki na burudani kwa ujumla wa Dar es Salaam na vitongozi vyake, yupo mkali wa Bongo Fleva, Ali Kiba pamoja na kijana asiye na makeke mwenye kipaji cha hali ya juu, Aslay.
Lakini pia, kutakuwapo na wasanii wengine wakali hapa nchini wakiwamo Ben Pol, Jux, Vanessa, Nandy, Dogo Janja, Rostam, Darassa, Weusi na wengineo wengi, hasa wale ambao walipata nafasi ya kutumbuiza katika matamasha ya mwaka huu yaliyofanyika takribani miji 15 Tanzania Bara.
Pamoja na wasanii hao, Ali Kiba anayetamba na wimbo wake wa Seduce Me na Aslay ambaye ameonekana kuwateka wapenzi wa muziki nchini baada ya kutoa nyimbo mpya 13 ndani ya muda mfupi, tayari wameanza kuwa gumzo wakisubiriwa kwa hamu kuona watafanya nini hiyo Novemba 25.
Kati ya mambo yanayowafanya wasanii hao kusubiriwa kwa hamu, ni ubora wa kazi zao, lakini pia wakijitambulisha kama miongoni mwa wasanii wenye vipaji vya hali ya juu katika muziki, hasa katika kuimba.
Kwa upande wake, Ali Kiba ameonekana kubamba vilivyo na wimbo wake wa Seduce Me ambapo kila alipopanda jukwaani katika matamasha ya Tigo Fiesta mwaka huu, alikuwa akishangiliwa vilivyo.
Pamoja na Kiba, Aslay naye si mtu wa mchezo mchezo kama alivyojidhihirisha kwenye shoo za mikoani, hivyo ni wazi kuwa wakazi wa Dar es Salaam watakuwa wakisubiri kwa hamu kumwona akifanya vitu vyake pale Leaders Club Jumamosi.
Akitamba na nyimbo zake mpya za Pusha, Natamba, Mario, Danga, Rudi, Kidawa na nyinginezo, Aslay anatajwa kuwa msanii aliyeongoza kwa kupewa ushirikiano wa hali ya juu na mashabiki wakati wote wa tamasha la Tigo Fiesta, ambapo mashabiki walikuwa wakiimba naye na kucheza nyimbo zake kwa hisia kali.
Katika majukwaa yote aliyopanda jukwaani, idadi kubwa ya watu waliohudhuria shoo za tamasha hilo, waliimba pamoja na Aslay na mwisho wa siku, kumshangilia vilivyo kijana huyo aliyemeguka kutoka Bendi ya Yamoto.
Akizungumzia shoo zake zote za mikoani, Aslay anasema kuwa ile ya Arusha ndiyo ilikuwa ‘mambo yote’.
Anasema ikiwa ndiyo Fiesta yake ya kwanza mwaka huu, hakuamini jinsi mashabiki walivyompokea na kumpa ushirikiano wa aina yake kwa muda wote aliokuwapo jukwaani.
“Si kama katika mikoa mingine sikufanya vizuri au sikupokewa vizuri, bali Arusha ilikuwa ni ‘bab kubwa’, ikiwa ndio shoo yangu ya kwanza katika jukwaa la Tigo Fiesta mwaka huu, nilipokewa vizuri sana, watu waliimba pamoja nami na hivyo kunifanya niwe na mwanzo mzuri wa safari ya Fiesta mwaka huu,” anasema.
Aslay anasisitiza kuwa amejipanga vilivyo kuhakikisha anafanya shoo ya nguvu jijini Dar es Salaam Jumamosi kama ilivyo kawaida yake.
“Novemba 25 pale Leaders Club, Dar es Salaam ndio kilele cha Tigo Fiesta, nimejipanga kufanya mambo makubwa hivyo wapenzi wa muziki na burudani wajitokeze kwa wingi siku hiyo sitawaangusha hata kidogo,” anasema.
Juu ya tamasha hilo la funga msimu Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, anasema kuwa wakazi wa jiji hilo watarajie burudani ya aina yake kwani wasanii watakaopanda jukwaani, wamejiandaa vema kufanya mambo makubwa.
Mpinga alisema kwamba kwa kuwa lengo la tamasha hilo ni kutoa burudani halisi kwa wapenzi wa muziki na burudani kwa ujumla hapa nchini, kamwe hawatawaangusha wakazi wa Dar es Salaam kama walivyofanya kwenye maeneo mengine lilikopita tamasha hilo.
Anasema tamasha hilo ambalo ni la 16, limeshatimua vumbi katika miji ya Arusha, Musoma, Kahama, Mwaza, Tabora, Kigoma, Njombe, Iringa, Songea, Mbeya, Sumbawanga, Tanga, Moshi, Dodoma, Morogoro na Mtwara.
Anawataka wakazi wa Dar es Salaam kununua tiketi kwa Tigopesa ili kupata punguzo la asilimia 10, yaani kulipa Sh 9,000 badala ya 10,000.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Fiesta, Sebastian Maganga, alisema wakazi wa Dar es Salaam watarajie shoo kabambe na ya aina yake kutoka kwa wasanii wao wakali wa hapa nchini.
“Tutawaletea wasanii wenye hadhi kulingana na mapendekezo ya mashabiki husika wa mkoa huo, tena wale waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi,” anasema Maganga.
Credit – Bingwa
The post Aslay – Tigo Fiesta 2017 imenibamba sana appeared first on Mtembezi.
Chanzo http://ift.tt/2jO3Zn1 SOMA ZAIDI
0 Comments