AGAPE yaanza Mkakati wa Kuzuia Mimba na Ndoa za Utotoni, Shinyanga

Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP) la Mjini Shinyanga limekutana na wanafunzi na walimu wa shule za msingi Didia, Mwanono, Bugisi, Mwamalulu, Bukumbi na shule ya Sekondari Didia zilizopo katika kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuzuia ndoa na mimba za utotoni.

Kikao hicho kimefanyika leo Ijumaa Januari 19,2018 katika shule ya msingi Didia na kuhudhuriwa na baadhi ya wanafunzi walioambatana na walimu wao kutoka shule hizo.

Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE, Mustapha Isabuda alisema lengo la kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Didia Felister Meli,Kaimu Mtendaji wa kata William Nkuya ni kupanga mikakati ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni ili wanafunzi waweze kumaliza masomo yao vizuri.

Alisema wanafunzi waliohudhuria kikao hicho watakuwa viongozi wa wanafunzi wengine katika kupambana na ndoa na mimba za utotoni ambapo wataunda klabu kwa ajili ya masuala hayo zitakazopewa jina la “Tuseme Klabu”.

“Hatutaki kuona mwanafunzi anakatiza masomo kwa sababu ya kupewa mimba ama kuolewa, ni wajibu wetu wanafunzi, walimu ,serikali na wadau wote tushirikiane kupaza sauti ili watoto wetu watimize ndoto zao”,alieleza Isabuda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE John Myola alisema bado jitihada kubwa zinatakiwa kufanyika ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika jamii kwani baadhi ya matukio yamekuwa yakifanywa na ndugu wa karibu huku kesi za watoto zikifanywa dili na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

Kwa upande wake Secilia Kiza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga aliwataka wanafunzi kutofumbia macho vitendo vya ukatili na watoe taarifa katika vyombo vinavyotakiwa.

The post AGAPE yaanza Mkakati wa Kuzuia Mimba na Ndoa za Utotoni, Shinyanga appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini