TFF yatoa hukumu dhidi ya Viongozi hawa wa Soka Nchini

Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) imetoa hukumu dhidi ya viongozi wanne waliotuhumiwa kwa makosa ya kughushi na udanganyifu wa mapato kwenye mchezo namba 94 kati ya Ndanda FC na Simba uliochezwa Disemba 30,2017.

Kamati hiyo imemhuku Msimamizi wa Kituo cha Mtwara, Dunstan Mkundi kutojihusisha maisha na mpira wa miguu baada ya kumkuta na hatia ya kushindwa kuwasilisha fomu ya mapato ya mchezo huo ndani ya saa 48 , kutotoa maelezo ya kutosha kuhusu utata wa fomu mbili zilizoonyesha utofauti wa mapato,pamoja na kutosimamia mauzo ya tiketi zilizotumika.

Pia kamati imemfungia Katibu mkuu wa Chama cha soka Mtwara Kizito Mbano, kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kukutwa na hatia ya kughushi fomu ya marejesho ya mapato ya mchezo kwenye mchezo huo.

Katika hatua nyingine, Kamati imempa onyo Katibu Msaidizi wa Klabu ya Ndanda, Selemani Kachele kwa kushindwa kutoa uthibitisho wa kulipwa kwa deni la Ndanda wakati wa kuhesabiwa mapato ya mchezo huo.

Aidha, Kamati haikuendelea na tuhuma dhidi ya Mhasibu Msaidizi wa Simba, Suleiman Kahumbu baada ya Sekretarieti ya TFF kuamua kuondoa shauri dhidi yake kwa kuwa alitoa ushirikiano na kutosheka kuwa hana hatia na badala yake alitumika kama shahidi wa upande wa washtakiwa.

Kamati imeiomba Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kutafuta njia bora ya kuimarisha udhibiti wa mapato kwa kuongeza uwajibikaji wa uwazi kwa wadau wote,Vilevile Kamati inashauri Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kuharakisha mchakato wa kukusanya mapato yake kwa njia za kielektroniki ili kuziba mianya ya upotevu.

The post TFF yatoa hukumu dhidi ya Viongozi hawa wa Soka Nchini appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini