Aliyekuwa Waziri wa JK ambaye alihamia Chadema atangaza kurudi CCM

MWANASIASA wa upinzani na aliyekuwa Naibu Waziri katika serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Goodluck Ole Medeye, ametangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi huku akidai kuwa ameamua kufanya hivyo kwa kuwa vitendo vya rushwa,

Hususan nyakati za uchaguzi, vimemalizwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, Ole Medeye alisema kilichomkimbiza CCM mwaka 2015 na kujiunga na Chadema ni vitendo vya rushwa katika mchakato wa kupata wagombea wa chama hicho tawala.

Alisema anafurahi kuona sasa vitendo hivyo havipo ndani ya CCM baada ya kudhibitiwa na Rais Magufuli.Ole Medeye alikuwa mmoja wa wabunge watano wa CCM waliojiunga na Chadema Agosti 12, 2015 wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Monduli). Ole Medeye aliteuliwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania nafasi ya Uspika wa Bunge baada ya Uchaguzi Mkuu.

Wengine waliohama pamoja na Lowassa ni Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) na mbunge wa viti maalum, Esther Bulaya ambaye sasa ni mwakilishi wa wananchi wa Bunda Mjini (Chadema).

Hata hivyo, Ole Medeye alihama Chadema kabla ya mwaka kumalizika na kujiunga na UDP kinachoongozwa na John Cheyo Juni 12, 2016.

Medeye alisema alihamia UDP kwa kuwa inasimamia haki na demokrasia na kwamba yeye alikuwa akitaka demokrasia ya kweli na jukwaa la haki katika kuleta haki na maendeleo kwa Watanzania.

Aliiambia Nipashe juzi kuwa alikaa chama hicho cha ‘Bwana Mapesa’ kwa miezi mitatu tu hata hivyo, kwa kuwa “nilikwenda kufanya kazi maalum.”

Na sasa, Ole Medeye amesema ameamua kurejea CCM kwa kuwa kila mwanachama anayo fursa kushiriki uchaguzi, ikiwamo kugombea nafasi yoyote bila kutoa rushwa na akashinda.

“Mimi sijawahi kuwahonga watu ili wanichague,” alisema Ole Mideye na “wakati huo CCM kulikuwa na rushwa sana; ndiyo maana nikaamua kukimbia.

“Lakini kwa sasa hakuna tena kitu kama hicho, hivyo nimeamua kurejea CCM.”

Ole Medeye alisema katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2020, anataka kurudi na kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya ubunge.

ELIMU BUREMbali na kutangaza kuhama upinzani na kurejea CCM, Ole Medeye pia aliiambia Nipashe kuwa kuna haja ya kurekebisha Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambayo inatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Alisema ni vizuri sera hiyo ikarekebishwa ili elimu ya kidato cha tano na sita nayo iweze kunufaika kwa kuwa wanafunzi wa ngazi hiyo kwa sasa hawaguswi.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa kusimamia vizuri sera hiyo ambapo Serikali imekuwa ikitoa takriban Sh. bilioni 20 kila mwezi ili kufanikisha watoto wetu kuelimika.

Ole Medeye pia alimpongeza Rais Magufuli kwa msisitizo wake wa mapema wiki hii ambapo alipiga marufuku michango ya aina yoyote shuleni.

Mbunge wa zamani wa Arumeru huyo anakuwa waziri wa pili wa serikali ya ‘JK’ kurejea CCM baada ya kutoka kwa muda.

Novemba 15, mwaka jana Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha alirejea CCM baada ya kujiondoa Chadema aliyoitumikia kwa miaka miwili.

Masha alikuwa Mbunge wa Nyamagama miaka ya 2005-2010 na baadaye kushindwa katika Uchaguzi Mkuu.

Credit – Nipashe

The post Aliyekuwa Waziri wa JK ambaye alihamia Chadema atangaza kurudi CCM appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini