Dondoo muhimu kuhusu matumizi sahihi ya muda kazini

MARA nyingi kinachowatofautisha watu waliofanikiwa na wale ambao hawajafanikiwa ni matumizi sahihi ya muda.

Muda ni moja ya rasilimali muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Kitu kibaya kuhusu muda ni ukweli kuwa ukishapita huwa haurudi tena. Hii inatukumbusha kuelewa umuhimu wa matumizi sahihi ya muda na kuhakikisha haupotei.

Katika mazingira ya kazi, matumizi mazuri ya muda yanapaswa kupewa nafasi kubwa ili kuongeza ufanisi na kujipunguzia msongo wa mawazo usio wa lazima.

Watu wanaofanikiwa katika kutumia muda wao vyema hufurahia shughuli zao na kumudu vyema mahitaji yao mengine nje ya kazi wanazofanya.

Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia katika kutumia muda vizuri;

Weka na kuzingatia vipaumbele

Katika majukumu yetu si kila kitu kina uzito sawa na kingine.

Yako mambo yanayotakiwa kufanywa kwanza kabla ya mengine. Hii inatukumbusha kuwa ni vyema kuhakikisha unaainisha shughuli au mambo unayotaka au unatarajia kufanya na kisha unayapanga kwa umuhimu wake.

Hii itakupa fursa ya kuyafanya yale yenye umuhimu na haraka zaidi ili kuokoa muda wako ambao pengine ungeutumia kwenye mambo yasiyo ya msingi.

Katika utekelezaji wa majukumu yako, anza na yale yenye umuhimu na haraka zaidi kisha yafuate yale yenye umuhimu sana lakini hayana haraka sana.

Ukishamalizana na haya ni vyema, kufanya yale yenye haraka sana lakini umuhimu mdogo. Yale yenye umuhimu mdogo lakini hayana haraka sana, unaweza kukaimisha kuyaacha mpaka utakapoona yanafaa.

Timiza moja kabla ya lingine

Imekuwa kawaida kwa wengi kuanza jambo moja na kisha kwenda kufanya lingine kabla lile la kwanza halijakamilika. Huku ni kupoteza muda na nguvu bila sababu ya msingi. Kama unaweza kufanya jambo moja kwanza na kulimaliza kabla haujaenda kwenye jambo lingine, ni vyema kulikamilisha kwanza na kisha lifuate lingine.

Kukamilisha jambo moja kunakuongezea hamasa inayoweza kukusukuma kufanya jambo lingine. Kuachia jambo njiani huongeza viporo vya kazi ambavyo huongeza msongo wa mawazo na kukuondolea umakini unapokuwa unafanya mambo mengine.

Jifunze kusema hapana

Kwa kawaida watu wanaokubali kila wanachoambiwa wafanye huonekana wenye adabu, heshima na utii. Watu hawa pia huonekana wenye upendo kwa wengine kwa kuwa na moyo wa utayari na kupenda kusaidia wengine.

Kwa upande mwingine watu hawa hujikuta kwenye majuto ya kukubali kwao pale wanapoelemewa na majukumu na kushindwa kuyatimiza kwa wakati. Jambo la msingi, jifunze kusema hapana pale unapoona huna muda wa kutosha, uwezo au motisha wa kufanya kile unachoombwa kufanya.

Wakati mwingine unaweza kuongezewa majukumu na bosi wako, lakini usidhani kuwa wao hawawezi kuambiwa hapana. Tafuta lugha nzuri ya kutoa maelezo na kuthibitisha kuwa kuongezeka kwa majukumu kutaathiriufanisi na ubora wa kazi husika, hivyo acha uoga.

Epuka vitu visivyo vya msingi

Tunapokuwa tukitekeleza majukumu yetu kuna mambo mengi ambayo huingilia na kupunguza kasi na umakini tunaouweka kwenye shughuli husika. Ukigundua kuwa kuna vitu vya namna hii, jifunze kuviepuka au tenga muda wa baadaye wa kuvifanya.

Inawekezana ni soga na mrafiki, matumizi ya simu au mambo mengine yanayoweza kusubiri. Pamoja na hayo, ukumbuke kuwa kazi zetu hazitakiwi kutuweka mbali na jamii inayotuzunguka.

Jifunze kukabili msongo wa mawazo

Maisha yanaleta changamoto mbalimbali. Changamoto hizi zinaweza kutoka nyumbani, mtaani, kwa marafiki, familia na hata kwenye kazi yenyewe.

Changamoto hizi hutuathiri kisaikolojia na kufanya tushindwe kuweka umakini katika shughuli tunazofanya.

Ni muhimu kuepuka mazingira yanayoweza kusababisha kuwa katika hali ya namna hii na pale inapokuwangumu kuepukika, tujue namna bora ya kukabiliana nayo.

Msongo wa mawazo ni moja ya mambo yanayochangia sana katika kupotea muda wetu tunaoutumia, hivyo tuwe makini kuepuka na kuukabili pale unapotokea.

Jifunze kusamehe

Migogoro kazini ni moja ya mambo ya kila siku. Kwa kuzingatia ukweli kwamba taasisi ni watu na watu wanatofautiana kwenye mitazamo, mawazo, fikra na mambo mengi, ni jambo la kawaida sana kukosea nakukosewa.

Hali hii ikitokea huumiza na kiwango cha maumivu hutofautiana kati ya mtu na mtu kwa sababu mbali mbali.

Unapokosewa hakikisha haichukui muda wako mwingi kuliwaza suala hili.

Kuwa muwazi kueleza pale unapoona umekosewa lakini usikae na jambo kwa muda mrefu hata kama haujaombwa msamaha.

Kumbuka pia suala la muhimu zaidi ni kujisamehe wewe mwenyewe pale unapoona umefanya uamuzi aujambo lisilo sahihi. Kuyawaza yale yaliyotokea na hauwezi kuyabadilisha ni kupoteza muda.

Omba msaada

Watu wengi wanakufa na tai shingoni katika maeneo ya kazi huku kukiwa na fursa ya kusaidiwa kwa namna mbalimbali pale mtu anapokwama kwenye jambo fulani. Inawezekana kabisa kazi uliyopewa imekushinda na huwezi kuendelea lakini umeng’ang’ania kujaribu tena na tena wakati unafahamu fika kuwa kuna mtu ana ujuzi au ufumbuzi wa tatizo hilo.

Usipoteze muda wako bila sababu ya msingi kwani unaweza hata kuharibu kazi yenyewe wakati kuna mtu angeweza kuwa msada kwako.

Kukosa ujuzi wa kitu fulani kunaweza kuwa kikwazo lakini wakati mwingine ni kuelemewa tu na ukubwa au wingi wa kazi. Jijengee utamaduni wa kuzungumza na wenzako ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kukusaidia ili umalize majukumu yako kwa wakati.

Mwisho, muda unaoutumia kazini unaathiri muda unaoutumia nyumbani au katika shughuli nyingine nje ya ofisi yako. Katika kupangilia matumizi yako ya muda kumbuka kufikiria wengine pia.

Ajira au kazi unayofanya isiwe kikwazo cha kushindwa kupata muda na familia au marafiki zako.

Kumbuka pia kupata muda wa kupumzika ili unaporejea kwenye shughuli zako urejee kwa kasi na motisha wa kazi.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe anapatikana kwa 0659 08 1838, kelvinmwita@gmail.com,

The post Dondoo muhimu kuhusu matumizi sahihi ya muda kazini appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini