Kamishna wa Madini aagizwa Kuanzisha Ofisi ya Madini Wilayani Ruangwa

Kamishna msaidizi wa madini kanda ya kusini Bw. Mayigi Makorobela ameagizwa kuanzisha haraka ofisi ya Madini Wilayani Ruangwa ikiwemo kupeleka wataalamu ili kurahisisha huduma za kitaalamu kwa wachimbaji wadogo ikiwemo elimu ya usalama kazini.

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Namungo Kata ya Megembekenyela wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisema kuwa Wizara ya Madini imeamua kuanzisha ofisi hiyo kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa hivi karibuni wakati alipokuwa ziarani Mkoani humo ambapo alibaini kuwa wachimbaji wadogo wanapata kadhia kubwa kutokana na umbali wa ofisi kwani wanalazimika kutumia zaidi ya kilomita 45 kuzifikia ofisi za madini zilizopo Wilayani Nachingwea.

Alisema kuwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa anawapenda wachimbaji wadogo nchini ambao hata hivyo Rais Dkt John Pombe Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu alibainisha kukusudia kuwanufanisha watanzania kupitia rasilimali zao ikiwemo madini.

“Mhe Rais Magufuli anataka wananchi wote wanaoishi karibu na mgodi kunufaika na rasilimali zao, nyote mtakuwa mashahidi, tangu nchi iliporuhusu uchimbaji wa madini hakuna manufaa ya moja kwa moja kwa watanzania badala yake madini yamekuwa yakinufaisha mataifa mengine ambayo baadaye tunayapigia magoti kuyaomba msaada” Alikaririwa Mhe Biteko huku akipigiwa makofi na wananchi waliohudhuria katika mkutano huo

Mhe Biteko alisema kuwa lengo la kuanzisha ofisi ya madini katika Wilayani hiyo ya Ruangwa ni kuwarahisishia wachimbaji kuwa na jukumu moja la kuchimba na kuuza rasilimali wanazozipata kwani watakuwa sehemu ya kuchagiza maendeleo sambamba na kuinufaisha serikali kutokana na ulipaji kodi.

Aliwasihi wachimbaji hao kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwani tangu ameingia madarakani katika kipindi kifupi ameimarisha nidhamu mpya kwa kila mtanzania na usimamizi madhubuti wa rasilimali za Taifa.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Biteko ameipongeza kampuni ya uchimbaji dhahabu na Green Garnet ya Gemini Exploration & Mining Services (GEMS) ambayo ni kampuni ya wazawa kwa kufanya kazi kwa kufuata vyema sheria na taratibu za uchimbaji.

Alisema kuwa kampuni zingine zinapaswa kujifunza kwa kampuni hiyo ya GEMS kutokana kulipa kodi mbalimbali kwa uwazi na ushiriki wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya, Maji, sekta ya elimu sambamba na michezo

The post Kamishna wa Madini aagizwa Kuanzisha Ofisi ya Madini Wilayani Ruangwa appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini