Avintishi alivyojinyakulia minoti ya pesa kutoka kwa JPM

Mwanamke aliyejitambulisha kwa jina moja la Avintishi,  amejitoa kimasomaso na kumueleza Rais John Magufuli kuhusu kero wanayopata wafanyabiashara ndogondogo ikiwamo kunyang’anywa bidhaa zao.

Mama huyo alimwambia Rais Magufuli jana katika uzinduzi wa kiwanda cha Sigara cha Philip Morris, Morogoro.

“Wanatunyang’anya bidhaa zetu, na sisi hatuna mtu wa kutusaidia, wanapochukua, wanatutoza fedha na wanachukua bidhaa. Na umri huu hatuwawezi vijana wadogo,” alisema mama huyo.

Baada ya kueleza hayo, Rais alimuita Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, John Mugarula kujibu kero zilizoibuliwa na mama huyo.

Mkurugenzi huyo, alisema wanawaondoa wafanyabiashara hao kwa sababu wametengewa maeneo maalumu na aliibua pia suala la kipindupindu kuwa ni sababu ya kuwaondoa wafanyabiashara hao.

Baada ya hapo Rais, alimuhoji mama huyo, ni kiasi gani alitozwa na askari mgambo wa manispaa, mama huyo akaeleza kuwa alitozwa Sh200, 000.

Rais alihoji tena, iwapo mama huyo anamkumbuka askari mgambo aliyemtoza kiasi hicho?

“Kwa sababu ya kitete na woga, siwezi kumkumbuka,” amejibu mama huyo.

Baada ya kusema hayo, Rais alimpa mama huyo fedha na kumtaka mkurugenzi kumpa kiasi kingine cha fedha mama huyo.

Kadhalika, Rais aliagiza kuanzia leo, wafanyabiashara hao wasibughudhiwe kwa sababu ni watoto wa maskini.

Wageni wengine waliokuwapo katika uzinduzi huo, akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM) Getrude Rwakatare, waliinuka na kumchangia fedha mama huyo.

The post Avintishi alivyojinyakulia minoti ya pesa kutoka kwa JPM appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini