Masauni asisitiza onyo kwa wanaotaka kuandamana

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni amesema watu wanaopanga kufanya maandamano wajaribu waone.

Amesema hawatakubali kuruhusu watu wachache waitoe Serikali kwenye mstari wa maendeleo kwa kuibua ajenda zisizo na msingi.

Masauni ametoa kauli hiyo wakati akipokea vituo sita vya polisi vinavyohamishika kutoka katika kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola, hafla iliyofanyika kituo cha Polisi cha Oysterbay.

“Serikali imejitahidi kukabiliana na changamoto mbalimbali, lakini kuna baadhi ya watu wapo ndani ya nchi na wengine nje ya nchi ni maadui wa mafanikio haya na wanataka kututoa katika ajenda,” amesema.

“Nasema nafasi hiyo hawana, kamwe Serikali na wizara hii hatutaruhusu mtu yeyote atutoe kwenye mstari.”

Machi 6, zilisambaa taarifa zinazodai kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo ametekwa, lakini siku iliyofuata alionekana eneo la Mafinga mkoani Iringa na polisi ilitoa taarifa ya kuwa alifika mwenyewe kituoni saa moja na kuripoti kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwaambia wanahabari kuwa Nondo hakutekwa kama anavyodai bali ‘alijiteka’ mwenyewe.

Naibu waziri huyo alidai kuwa kuna mwingine anawahamasisha Watanzania kutozingatia fursa mbalimbali zilizopo ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa badala yake anawataka kushiriki maandamano.

“Limeshasemwa, mimi nasisitiza kama kuna wapuuzi wawili watatu wajaribu waone. Hatuwezi kuacha ajenda za msingi za maendeleo tukashughulika na vitu vya kipuuzi,” amesisitiza Masauni.

Amesema kuwa nchi imebadilika na mambo makubwa yamefanyika chini ya uongozi Rais John Magufuli na kuwataka Watanzania kumuunga mkono katika jitihada za kuwaletea maendeleo.

Kuhusu vituo hivyo, Masauni ameishukuru kampuni hiyo na kusema vitasaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

Mbali na hilo, amesema Serikali ina mkakati wa kuhakikisha vituo kama hivyo vinapatikana katika mipaka mbalimbali ili kudhibiti wimbi la wahamiaji.

Amesema vituo vyote vilivyotolewa na Coca Cola vitakuwa Kinondoni kwa sababu ya changamoto za kiuhalifu zilizopo, ingawa hivi sasa zimeanza kupungua kutokana na jitihada mbalimbali.

Mkuu wa operesheni na mafunzo wa Jeshi la Polisi, kamishna Nsato Marijani alimuhakikishia Masauni kuwa wapo imara na matukio ya uhalifu yamepungua.

“Hakuna tishio lolote ambalo lipo nje ya uwezo wa polisi kulikabili. Kama mtu ana wasiwasi na uwezo wetu basi asiyejua kufa achungulie kaburi, sisi tupo imara na tutaendelea kuwa imara,” amesema.

Kamishna Marijani amesema vituo hivyo vinavyohamishika vitakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na vituo vikubwa vya polisi ili kurahisisha utendaji kazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Murilo amesema vituo hivyo ni vya kisasa na vitakuwa na huduma zote muhimu kwa askari tofauti kidogo na vile vya awali.

The post Masauni asisitiza onyo kwa wanaotaka kuandamana appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini