JPM ainyooshea kidole TRA

WAZIRI wa Fedha na Mipango na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wameagizwa kuhakikisha wanaondoa kero za kodi, ili kutoa hamasa kwa wananchi kulipa kodi kwa manufaa ya taifa.

Agizo hilo lilitolewa jana Ihumwa, Dodoma na Rais John Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi la sehemu ya pili ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) ambao utaanzia Morogoro hadi Makutupora, Dodoma.

Rais Magufuli alisema ni vyema TRA ikaangalia kodi inazotoza kwa kuwa inawezekana zingine ni kubwa mno kuliko miradi ambayo wananchi wanatekeleza au kuwekeza.

“Badala ya kuwa motisha kwa walipakodi inakuwa kero kwa walipakodi. Badala ya kulipa kodi wanabuni mbinu za kuwepa kodi wakati wangeelimishwa vizuri wangeweza kulipa kodi. Kwa hiyo, TRA mjipange vizuri,” alisema.

Rais Magufuli aliongeza: “Tulizungumzia suala la kodi za nyumba mmeenda mnatoza Sh. 600,000 hadi milioni moja kwenye nyumba wakati tuliwaambia mpige ‘flat rate’ ambayo itakuwa motisha, ili Watanzania wengi wawe wanalipia majengo yao.”

Alisema kuna watendaji TRA siyo watu wazuri na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakiipaka matope serikali kwa kusema hiyo ni dhana ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Kumbe wao wanatafuta kazi ya kuliibia taifa. Kamishna wa TRA, Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu mkalisimamie hili ili kulipa kodi isiwe ni kero bali iwe heshima kwamba mwananchi amelipa kodi kwa heshima ya nchi yake,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka Watanzania kuendelea kulipa kodi ili kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma mbalimbali za jamii.

“Pamekuwa na mtindo mtu anapoenda kununua bidhaa anapewa risiti ya bei ndogo badala ya risiti anayotakiwa kupewa, mtoa risiti na mpokea risiti wote wanaiibia serikali, wanachelewesha maendeleo ikiwamo ya kujenga reli, nawaomba Watanzania muwe wazalendo,”alisema.

Aliwataka Watanzania kudai risiti kila wanaponunua bidhaa na kila huduma lazima iwe na risiti.

“Suppliers’ (wasambazaji) kwenye vyombo vya ulinzi na usalama lazima risiti zitolewe, kwenye shule lazima risiti zitolewe, pia magereza ingawaje bado ni aibu kuwapelekea wafungwa vyakula wakati wanatakiwa wajilishe wenyewe lazima risiti zitolewe,” alisisitiza.

Alisema ujenzi wa reli hiyo ni wa awamu tano ambapo zitahitajika jumla ya Sh. trilioni 15, ili ifike Mwanza, Kigoma na kuunganishwa na Kigali na Burundi.

Rais Magufuli pia aliwataka Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuimarisha amani.

Alisema fursa zimekuja kwa wakazi wa Dodoma hasa kutokana na ujio wa serikali na kwamba fursa nyingi za uchumi zimeenda hususan kwenye ujenzi.

“Leo (jana) nilikuwa nazungumza na Balozi wa Morocco kuhusu salamu zilizotoka kwa Mfalme wa Morocco, wanaanda utaratibu wa kujenga uwanja mkubwa wa mpira hapa Dodoma na wataalamu wetu wanatakiwa kupeleka michoro wiki ijayo, hizi zote ni fursa,”alisema.

The post JPM ainyooshea kidole TRA appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini