JPM atangaza fursa 8 kabambe

RAIS John Magufuli ametangaza fursa nane kabambe ambazo serikali yake ya awamu ya tano imepanga kuwaletea wananchi wanyonge wa Tanzania, ikiwemo ajira.

Katika suala hilo la ajira, Rais Magufuli amesema serikali yake imejibu suala la uhaba wa ajira nchini kwa vitendo kwa kutengeneza ajira takribani milioni moja kutokana na kuanzisha miradi mbalimbali nchini. Kati ya miradi hiyo, Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) pekee umezalisha ajira takribani 30,000 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 600,000 zinazohusu watu mbalimbali watakaojiajiri kwa kutoa huduma kwa wafanyakazi katika mradi huo.

Rais Magufuli alitambia mafanikio iliyopata serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo ya kisasa katika eneo la Ihumwa, umbali wa kilometa 15 kutoka Mjini Dodoma. Alitaja mifano ya miradi mingine inayozalisha ajira kuwa ni pamoja na mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, zaidi ya ajira 15,000, mradi wa Umeme Rufiji ajira 20,000, barabara mijini ajira 30,000, barabara vijijini ajira 70,000 na miradi ya umeme vijijini, ujenzi wa meli na miundombinu mingine inayozalisha mamilioni ya ajira.

“Pamoja na serikali kuzalishaji ajira hizo katika sekta mbalimbali, Watanzania mnatakiwa msichague kazi, hata kama mnasema vyuma vimebana mkifanya kazi havitabana tena kwani asiyefanya kazi hastahili kula na asipokula na afe,” alisema huku akishangiliwa na watu. Akizungumzia mradi wa reli ya SGR, Rais Magufuli alisema reli hiyo haipo popote katika Afrika Mashariki kwani wengine waliiga wakashindwa kujenga kama Tanzania ambayo inajenga kwa kutumia fedha zake za ndani. Alisema; “Watanzania mnatakiwa kujivunia ujenzi wa reli hii, kwani mimi ni kiongozi ninayepita lakini yenyewe itabaki, kama ambavyo Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Kikwete walipita na sasa na mimi natapita, lakini miundombinu itabaki ni kwa manufaa ya vizaji vijavyo.”

Rais Magufuli alisema, utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, baadaye Kigoma, Rwanda na Burundi, unatakiwa kusimamiwa kwa karibu na wizara hivyo akatoa mwito kwa wizara, mhandisi mshauri na mkandarasi mjenzi kuhakikisha unamalizika kwa wakati. Ukombozi kwa watumishi waliohamishiwa Dodoma Alisema kutokana na reli hiyo Tanzania na hasa Dodoma itakuwa kama Ulaya ambako mtu anaishi Dar es Salaam na anafanya kazi Dodoma, kwani atahitaji saa tatu tu kusafiri kutokana na kasi ya kilometa 160 kwa saa katika umbali wa kilometa 522.

“Treni hii ya umeme itawezesha watu kufanya kazi Dodoma lakini wakaishi Dar es Salaam. Kunaweza kuanzishwa kwa treni ya express (haraka) yenyewe ikawa inatoka mapema ili wafanyakazi waweze kuwahi. “Lakini pia itawasaidia wafanyabiashara kwenda kuuza mboga Kariakoo Dar es Salaam kwa kusafiri kwa saa tatu, halafu baada ya kuuza mboga wakawatembelea ndugu na jamaa Mbagala na Kigamboni na kurejea Dodoma.”

Alisema reli hiyo ambayo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma itagharimu Sh trilioni 7.062 na hadi Mwanza Sh trilioni 15, inajengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania, hivyo kuagiza kila mtu alipekodi ili kujenga miundombinu hiyo. “Tayari serikali imeshalipa malipo ya awali ya Sh bilioni 500 ambayo ni asilimia 15 kabla ya kuanza ujenzi, ninachotaka ni kuhakikisha inaharakishwa na ikiwezekana imalizike kabla ya muda wa miezi 36 ya Mkataba,” alisema.

The post JPM atangaza fursa 8 kabambe appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini