Mbunge CCM ataka kamati ichunguze usalama taifa

MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, amewasilisha kwa Katibu wa Bunge barua ya kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kuundwa kwa kamati teule kuchunguza matukio mbalimbali kuchunguza matukio yanayotishia pamoja na mambo mengine, “usalama wa taifa letu.”

Bashe (CCM) aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter juzi kuwa mbali ya masuala ya usalama wa taifa, atataka kamati yeule ya bunge hiyo ichunguze pia masuala yanayotishia umoja na mshikamano wa taifa.

“Leo asubuhi nimewasilisha Kwa Katibu wa Bunge barua ya kusudio la kuwasilisha Hoja Binafsi ya kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza matukio mbalimbali yanayoonesha kutishia umoja, usalama na mshikamano wa Taifa letu,” alisema Bashe katika ujumbe huo.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, alilieleza gazeti la Nipashe kwa njia ya simu kuwa hajapokea taarifa ya kusudio la mbunge huyo.

“Sijapokea barua hiyo… ndiyo kwanza nasikia (kutoka kwako),” alisema katibu huyo.

Barua ya Bashe kuhusu pendekezo hilo ambayo imesambaa kwenye mitandao zaidi ya kijamii inaonyesha amechukua uamuzi huo katika kutimiza majukumu yake kama Mbunge.

Ni “kwa mujibu wa Ibara ya 63(2) ya Katiba ya nchi kwa kuzingatia kanuni za huduma za Bunge toleo la Januari 2016, mahususi kanuni ya 55 ya fasili ya (1), (2) zikisomwa,” alisema.

Barua hiyo ilisema pamoja na kanuni ya 120 fasili (1) mpaka ya (4) “ninakusudia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano ujao wa Bunge la kumi na moja (11) kuunda kamati teule ya Bunge kuchunguza matukio mbalimbali yanayoonyesha kutishia umoja, usalamana, mshikamano wa Taifa letu.”

Mkutano ujao wa Bunge unatarajiwa kuanza Jumanne ya Aprili 3.

Ametaja matukio muhimu ya kutazamwa kuwa ni kusinyaa kwa demokrasia na haki za raia, kupotea, kutekwa na kuuwawa kwa raia katika chaguzi mbalimbali na matukio ya uhalifu katika siasa.

Mengine ni kupigwa risasi na kuumizwa kwa raia ndani ya nchi na kikundi cha watu wasiojulika, mauaji ya viongozi wa kisiasa wanaotokana na vyama halali vya siasa nchini na ukandamizaji wa uhuru wa raia kutoa maoni, kukosoa na kushauri.

Wasiwasi mwingine wa Bashe ni madai ya matumizi mabaya ya sheria na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya nchi, haki za kikatiba na kisheria za vyama vya siasa kutoheshimiwa na tuhuma dhidi ya vyombo vya usalama na matumizi ya silaha za moto kwa raia.

“Nimechukua hatua hii kutokana na matukio tajwa hapo juu kujirudia na raia kuendelea kuwa na hofu na ongozeko la mgawanyo katika jamii kwa kuwa jambo hili muhimu katika kulinda usalama wa Taifa letu na jukumu la msingi la Bunge ni kusimamia serikali kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 63(2) na tuhuma zote hizi zinagusa moja kwa moja taasisi zilizo serikalini,” anasema Bashe.

“Nimeona kuna umuhimu wa jambo hili kupewa fursa kujadiliwa ndani ya Bunge na kuundwa Tume Teule ya Bunge ambayo itafanya uchunguzi na kuwasilisha taarifa ndani ya Bunge ili kulinda usalama wa Taifa letu.”

The post Mbunge CCM ataka kamati ichunguze usalama taifa appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini