YAJAYO YANAFURAHISHA! YANGA YAIFIKIA SIMBA KILELENI VPL

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, Yanga leo wameendeleza wimbi la ushindi katika harakati zao ngumu za kuutetea ubingwa huo baada ya kuitandika Stand United ya Shinyanga kwa mabao 3-1.

Wakiuanza mchezo huo kwa kasi, Yanga waliandika bao la kwanza mapema mnamo dakika ya 6 ya mchezo ambalo lilipatikana baada ya mpira wa krosi uliopigwa na Yusuf Mhilu kumgonga mlinzi wa Stand, Ally Ally na kujaa nyavuni.

Yanga waliendelea kulisakama lango la stand na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Ibrahim Ajibu baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa kijana wa Ngorongoro Heroes Maka Edward na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa inaongoza mabao 2-0.

Kipindi cha pili hakikua kizuri kwa vijana wa Jangwani wanaonolewa na Mzambia George Lwandamina kwani  Wapiga debe wa Stand waliwashambulia vilivyo wakiongozwa na washambuliaji wao wa kigeni Ndikumana Laundry na Bigirimana Blaise Babikakuhe ambao walilisakama lango la Yanga kwa muda mrefu mara nyingi uimara wa mlinda mlango Youthe Rostande uliwanyima faida.

Hata hivyo Stand walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi mnamo dakika ya 84 ya mchezo likifungwa na kijana mwingine wa Ngorongoro Heroes Vitalis Mayanga.

Bao hilo lilionekana kufufua matumaini ya Stand kuibuka na point katika mchezo huo lakini Obrey Chirwa alizima ndoto hizo dakika moja baadae baada ya kuiandikia Yanga bao la tatu kwa shuti kali.

Kwa matokeo hayo sasa Yanga wamerejea katika nafasi ya pili wakiwa na alama 46 sawa na Simba huku Yanga wao wamewatangulia Simba kwa mchezo mmoja.


Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini