Hizi Hapa Sababu za Mtoto Kuzaliwa kabla ya Wakati "Njiti"


Kila mwaka watoto takribani milioni 15 huzaliwa kabla ya miezi tisa yaani njiti na idadi hii imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Ni moja kati ya sababu inayochangia kwa wingi vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria takribani watoto milioni moja walipoteza maisha kutokana na tatizo hili mwaka 2015, hata hivyo, inaelezwa robo tatu ya vifo hivyo vingeweza kuzuilika. Kwa kila watoto kumi wanaozaliwa, mmoja kati yao ni njiti. Na pia, takribani watoto milioni moja hupoteza maisha kila mwaka kutokana na tatizo hilo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na WHO.

Je nini chanzo cha watoto kuzaliwa Njiti?

Wanawake wenye historia ya kupatwa na uchungu mapema, wapo katika hatari ya kuzaa njiti ukilinganisha na wasio na historia hiyo.

Pia, kuwa na mimba yenye zaidi mtoto mmoja huchangia kuzaa njiti. Utafiti mbali mbali uliofanyika, unaonyesha nusu ya watoto wanaozaliwa mapacha ni njiiti ukilinganisha na anayezalizaliwa peke yake.

Chanzo kingine ni kwa wanawake wenye matatizo katika maumbile ya mfumo wa uzazi, nao wapo katika hatari zaidi. Sababu nyingine ni maradhi katika njia ya mkojo, UTI, maradhi yanayosababishwa na ngono zembe ukiwamo Ukimwi, kisonono, kaswende na trikomonasi.

Tatizo la shinikizo la damu, kutokwa na damu katika sehemu za uzazi, mama kuwa na uzito mdogo au mkubwa kupitiliza kiasi wakati wa ujauzito, kujifungua mara kwa mara katika kipindi kifupi, kuchanika kwa mfuko wa uzazi na kondo la nyuma kabla ya wakati na kisukari cha mimba huchangia katika tatizo hili.

Mambo megine yanayochochea ni umri wa mjamzito. Inaelezwa wanawake wanaojifungua wakiwa chini ya umri wa miaka 18 wapo katika hatari ya kuzaa njiti kwani katika kipindi hicho mfumo wa uzazi unakuwa bado haujakomaa.

Wanawake walio na umri unaozidi miaka 35 wapo katika hatari pia kwasababu katika umri huu mkubwa, wengi wao huwa na maradhi chochezi kama kisukari na shinikizo la damu.

Matatizo ya kifamilia, msongo wa mawazo na ya kisaikolojia kama kupigwa na kuteswa wakati wa ujauzito, kufanya kazi za kusimama kwa muda mrefu ni moja ya mambo yanayochochea.

Dalili zinazoambatana na tatizo hili

Maumivu chini ya mgongo, yanayoweza kuwa ya kudumu au kuja na kuondoka na hayaondolewi kwa kubadilisha pozi.

Kutokwa na maji maji na damu sehemu ya siri yanayoashilia kupasuka kwa chupa. Kupatwa na uchungu zaidi ya mara nne ndani ya saa moja.

Mtoto njiti anaweza kukumbwa na matatizo gani

Matatizo ambayo huwakumba watoto wanaozaliwa njiti ni pamoja nay a kupumua, kwani wakati huu mfumo wa hewa huleta shida kwa sababu mapafu yanakuwa hayajakomaa.

Shida nyingine ni upande wa ulaji au unynyaji kutokana na mfumo changa wa chakula. Mara nyingine watoto hawa hupatwa na matatizo katika kusikia na kuona ambayo huchochewa na kuchelewa kwa ukuaji wa mfumo wa fahamu, hali hii huathiri ukuaji wa mtoto kwa ujumla.

Mambo muhimu ya kuzingatia

Hakikisha kipindi cha ujauzito hautumii vilezi, sigara na dawa za kulevya, hudhuria kliniki kwa ajili ya afya ya uzazi pamoja na kupima maradhi ya zinaa, pata muda wa kutosha wakupumzika kwa kujiepusha na kazi nzito na zinazohusisha kusimama kwa muda mrefu, pata lishe ya kutosha yenye virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mtoto na afya ya uzazi. Kujiepusha na mimba katika umri mdogo hasa chini ya miaka 18 na kuzingatia maagizo ya uzazi wa mpango kwa kuepuka kubeba mimba kila baada ya muda mfupi, hasa ulio chini ya miaka 2. Si jukumu la mama tuu, bali pia baba, katika kuutunza ujauzito ili kuepusha matatizo katika kipindi cha ujauzito.

Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini