Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeitaka Taasisi ya Twaweza kujieleza ndani ya siku saba kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kutoa matokeo ya utafiti bila ruhusa.
Barua hiyo ya Costech imesema, Twaweza waliomba kibali cha tafiti nne ambazo mmoja umekamilika na nyingine tatu bado zinaendelea.
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosambaa mitandaoni ikionyesha imesainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu, tume hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusajili na kutoa kibali cha tafiti zote za muda mfupi na mrefu zinazofanywa nchini.
Barua hiyo imedai kuwa mwishoni mwa wiki, kulikuwa na taarifa za Twaweza kutoa utafiti uliopewa jina la ‘Sauti za Wananchi’ ambao, tume haina rekodi zilizoruhusu kuchapishwa kinyume cha sheria.
“Kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 7 cha mwaka 1986, tume hiyo ndiyo yenye mamlaka kusajili na kutoa kibali cha kufanyika tafiti nchini,” imesema barua hiyo.
Taarifa kutoka Twaweza zinathibitisha taasisi hiyo kupokea barua kutoka Costech na kwamba wanaifanyia kazi.
Hivi karibuni Twaweza walitoa ripoti ya utafiti wa ‘Sauti za Wananchi’ ukielezea maoni ya wananchi kuhusu siasa nchini.
Utafiti huo umeonyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais anavyotekeleza majukumu yake tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments